Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatua kwa hatua mauaji ya Milembe wa GGML

Milembe Kuzikwa.jpeg Hatua kwa hatua mauaji ya Milembe wa GGML

Thu, 20 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Shahidi wa 13 wa upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa GGML, Milembe Suleman (43) aliyeuawa Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo kichwani, usoni na mikononi, ameeleza namna mauaji hayo yalivyofanyika.

Shahidi huyo ambae ni askari wa kitengo cha upelelezi G4742 Koplo Michael wa Kituo cha Polisi Sengerema mkoani Mwanza aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Genja Deus Pastory katika maelezo hayo mshtakiwa alikiri kumuua Milembe Suleman.

Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Merito Ukongoji, shahidi huyo ameieleza Mahakama kuwa Mei 5, 2023 alipokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Sengerema, Tito akimtaka kwenda kituo kidogo cha Polisi cha Nyakalilo kumkamata mtuhumiwa.

Akiambatana na mkuu wake wa kituo, alipofika Nyakalilo alipewa jukumu jingine la kuandika maelezo ya mtuhumiwa Genja Deus Pastory anayetuhumiwa kuhusika kwenye mauji ya Milembe Suleman.

Akitoa ushahidi kwa kusoma maelezo ya onyo ya mshtakiwa pamoja na mambo mengine, alidai kuwa Machi 2023 kwa tarehe asiyoikumbuka, asubuhi akiwa Bugalama mkoani Shinyanga akiwa mgonjwa aliazima simu na kumpigia kaka yake (mtoto wa baba mkubwa) na kumueleza hali yake.

Kaka yake huyo alimueleza amtafute Musa Ally ambaye naye alimtaka amtafute Safari Lubingo aliyekuwa na kazi ya kufanya na kwa kuwa hakuwa na fedha, alimtafuta Safari aliyemtaka kuja Geita ili wakafanye kazi.

Amedai kwa kuwa hakuwa na simu, Safari Lubingo alimtumia Sh215,000 kupitia simu ya Musa na kuanza safari ya kuja Geita na walipofika walipelekwa hadi nyumba ya kulala wageni ya Kisesa na kupewa kazi ya kumuua mwanamke kwa sababu alikuwa akimsumbua wifi yake na kumzuia asitumie mali za mumewe aliyeko Afrika Kusini.

Wakiwa Kisesa, aliingia mwanamke mwenye gari nyeupe na kuonyeshwa kisha kuelezwa dau la kazi ni Sh1.2 milioni na kisha kupewa namba ya simu ya tajili aliyeko Mwanza na walipowasiliana naye alimtumia Sh150,000 na Safari Lubingo akaongeza Sh50,000.

Kutokana na mazingira ya nyumba ya wageni Kisesa, walishindwa kutimiza azma yao, ndipo tajiri yao ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, Dayfath Maunga alimtaka kwenda Usagara, Mwanza Jumamosi arudi na Milembe Jumatatu iliyofuata.

“Nilienda hadi mwanza na Dayfath alichukua nyumba ya wageni ya Angel na Jumatatu asubuhi nilitoka kama tulivyokubaliana hadi stendi ya Usagara na kumkuta Dayfath akiwa na Milembe kwenye gari na kuomba lifti lakini aliniambia nilipie nauli Sh7,000 na nililipa tukaanza safari ya kuja Geita tukiamuacha Dayfath,” amesema.

Kwa mujibu wa amaelezo ya mshtakiwa huyo, wakiwa njiani alimuomba ashuke ili akakojoe lakini Milembe alikataa kwa madai kuwa hasimami njiani, hivyo azma yake ya kumchoma kisu ikashindikana na kusafiri hadi Geita, huku wakipiga stori za uchimbaji dhahabu na masuala ya uganga.

Baada ya kufika Geita Milembe alimpatia namba yake na siku iliyofuata alimpigia simu akimuuliza kuhusu waganga na kumtaka kumtafutia mganga mzuri na baada ya hapo, Genja alimpa ujumbe kaka yake Safari Lubingo aliyemkutanisha na Buchuchu Lugodisha ajifanye kuwa ni mganga wa kienyeji.

Ameeleza kuwa Dayfath (mshtakiwa wa kwanza) alimueleza eneo nzuri la kumuulia ni kwenye nyumba zake anazojenga na yeye mshtakiwa (Genja) alimpa mikakati mtu aitwae Masumbuko Sumbu pamoja na Buchuchu Lugondisha na kuwasiliana na Mirembe aliyewataka wakutane eneo la Shilabela.

Mei 24, 2023 walikutana kwenye eneo la nyumba anazojenga na kuchanganya dawa na maji na kuanza kumwaga kwenye nyumba kisha kurudi hotelini na tukampa maelekezo ya kununua maziwa chupa saba.

Mei 25, 2023 alipotoka kazini, Milembe alimpigia simu Genja ili wakamtengenezee dawa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Calfonia akiwa na Masumbuko na Buchuchu, waliingia chumba namba 27 kwa ajili ya kumpa dawa huku Genja akibaki mapokezi.

Shahidi huyo ameeleza kuwa kwa mujibu wa maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu baada ya kumaliza kumzindika dawa, walikubaliana saa 1:30 usiku kwenda tena kutengeneza dawa kwenye nyumba anazojenga na saa 12:30 jioni, alipiga simu na kutuma dereva bajaji awafuate na walipofika walianza kuchimbia dawa huku yeye mshtakiwa wa tatu akabaki amesimama kwa ajili ya kumuua.

Amedai kuwa saa tatu usiku, wakiendelea kuweka dawa kwenye nyumba hizo, alimtaka Milembe aliyekuwa na tochi achuchumae naye alitii kisha kuanza kumkatakata na jambia sehemu mbalimbali za mwili na alizidiwa akaanguka, ndipo alimkata tena sehemu za kichwani.

Amedai baada ya kukamilisha kazi, walitoka na kuficha jambia hilo kwenye majani karibu na nyumba, Buchuchu Lugodisha aliyekuwa na simu za marehemu, walipotoka waliona choo na kuamua kuzidumbukiza ndani ya choo.

Shahidi huyo ameeleza kwamba walimpa taarifa Dayfath, usiku huohuo walianza safari ya kwenda Sengerema na walipofika kwenye msitu waliamua kulala ambapo Dayfath (mshtakiwa wa kwanza) aliwatumia Sh810,000 na asubuhi ya siku iliyofuata alituma tena Sh200,000.

Amedai baada ya kupata fedha hizo waliondoka na kwenda kwa mganga aitwae Cecilia Macheni (mshtakiwa wa tano) kwa ajili ya kuoshwa ili waondoe mkosi.

Mei 5, 2023 akiwa saluni huko Sengerema, alikamatwa kwa tuhuma za kumuua Milembe Suleman.

Akiulizwa maswali na upande wa utetezi, Wakili Erick Lutehanga alitaka kujua kama mshtakiwa aliwasiliana na Dayfath ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, kwanini namba za simu za mtu huyo hazipo kwenye maelezo na kuelezwa kuwa shahidi huyo alikuwa akiandika anachosema mshtakiwa na kuwa alipoulizwa namba za simu alidai hakuzikariri.

Alipoulizwa kuhusu Musa Pastory na Musa Ally kama walishiriki na mshtakiwa kutenda kosa hilo, alidai wao hawakushirikishwa kwa kuwa walionyesha nia ya kutotaka kuendelea na jambo hilo.

Chanzo: Mwananchi