Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatimaye kigogo TPA apata dhamana

Madeni Kipande Madeni Kipande

Sat, 23 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande (66), anayekabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh4.2 bilioni ameachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti.

Mbali na Kipande, washtakiwa wengine ambao wapo nje kwa dhamana ni Peter Gawile (58), ofisa rasilimali watu wa TPA, Casmily Lujegi (65) na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA, Mashaka Kisanta (59), Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi na Kilian Chale (51) Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Mkazi wa Mbezi Makabe.

Wakili wa Serikali, Yusuph Abood amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ramadhan Rugemarila ameieleza mahakama hiyo jana Ijumaa, Julai 22, 2022 kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya dhamana.

Hakimu Rugemalira amesema masharti ya dhamana kila mshtakiwa anatakiwa atoe kiasi cha Dola za kimarekani 185,790,84 sawa na zaidi ya Sh430 milioni au mali isiyohamishika na wawe na wadhamini wawili wanaoishi Mkoa wa Dar es Salaam watakaosaini bondi ya Sh400 milioni na washtakiwa hao wawasilishe hati zao za kusafiria.

Baada ya maelezo hayo, mshtakiwa huyo alikidhi mashrti hayo na yupo nje kwa dhamana.

Katika shtaka la kwanza, inadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi 2020 jijiniĀ  Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikula njama na kuisababishia TPA hasara.

Katika shtaka lingine kati ya Januari Mosi, 2015 hadi Februari 17, 2015 washtakiwa wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia dola za Marekani 1,857,908.04 .

Katika shtaka la mwisho, inadaiwa kati ya Oktoba Mosi 2014 na Oktoba Mosi,2020 maeneo ya TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washitakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP).

Inadaiwa walitangaza zabuni hiyo, bila kupata kibali cha bodi ya zabuni ya mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni za zabuni hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo jambo lililosababisha TPA hasara ya Dola za Marekani milioni 1.8 Sawa na zaidi ya Sh4.2 bilioni.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz