Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatima rufaa ya Mbowe, Matiko kujulikana kesho

29373 Mbowe3pic TanzaniaWeb

Thu, 29 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hatima ya usikilizwaji wa rufaa ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko itajulikana kesho Ijumaa.

Hiyo inatokana na leo Novemba 29, 2018 Jamhuri kuweka pingamizi la awali ikiwasilisha hoja tatu za kutaka rufaa hiyo itupiliwe mbali bila hata kusikiliza msingi wake.

Kufuatia hali hiyo, Mahakama Kuu kesho itatoa uamuzi wa pingamizi la Serikali iwapo litasikilizwa au litatupiliwa mbali.

Kama Mahakama hiyo itakubaliana na pingamizi la Serikali, rufaa ya Mbowe na Matiko itatupwa bila kusikilizwa na iwapo litatupwa Mahakama itaanza kusikiliza hoja ya rufaa hiyo na kisha kutoa uamuzi.

Uamuzi huo ni kuhusu usahihi wa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana Mbowe na Matiko.

Leo katika hoja ya kwanza ya kupinga rufaa ya kina Mbowe, Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango alisema kuwa taarifa ya kusudi la kukata rufaa hiyo si sahihi.

Alisema kifungu cha sheria kilichotumika katika taarifa ya kusudio la kukata rufaa hakiipi Mahakama mamlaka ya kuisikiliza kwa sababu siyo sahihi, hivyo inapaswa kutupiliwa mbali.

Katika hoja ya pili, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon alisema rufaa hiyo haijakidhi matakwa ya kisheria kifungu cha 362 (1) kuhusu mwenendo wa shauri kuambatanishwa katika rufaa.

Alisema mwenendo wa mambo mengi yaliyotokea siku za nyuma tangu kesi ya msingi ilipofunguliwa ambazo Mahakama ingezipata zingesaidia kuiongoza vyema kutenda haki.

Alisema masharti ya dhamana ambayo kwa mujibu wa kifungu hicho yanaweza kukatiwa rufaa lakini tangu yalipotolewa kati ya Machi na Aprili mwaka huu hayajawahi kukatiwa rufaa, kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa wala kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa.

Wakili Nchimbi alisema kwa hali hiyo inaonyesha kuwa wakata rufaa waliridhika na masharti hayo na hivyo haiwezekani kuja kuyaibua leo.

Baada ya upande wa Serikali kumaliza kutoa hoja zake za pingamizi, mawakili wa warufani, Peter Kibatala,  Dk Nshalla Lugemeleza na Jeremiah Mtobesya walitarajiwa  kujibu hoja hizo za pingamizi la Serikali.

Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai na Matiko wamekata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo.

Soma Zaidi: Polisi watanda mahakamani rufaa ya Mbowe ikisikilizwa

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi



Chanzo: mwananchi.co.tz