Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatima mabilioni ya Deci kutaifishwa kujulikana leo

55833 Dec+pic

Mon, 6 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hatima ya mali za  Kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (Deci), zikiwamo fedha taslimu Sh14.1 bilioni ambazo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) anaomba zitaifishwe, itajulikana leo Jumatatu Mei 6, 2019  Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itakapotoa uamuzi.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Jaji Stephen Magoiga kufuatia maombi yaliyofunguliwa na DPP, akiomba mali hizo zitaifishwe ziwe mali ya Serikali.

DPP alifungua maombi hayo Machi 2019, miaka takriban sita baada viongozi hao wa Deci kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam katika kesi ya jinai namba 109 ya mwaka 2009, kwa kosa la kuendesha biashara ya upatu kinyume cha sheria.

Viongozi hao wa Deci ambao walikuwa wachungaji, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kipentekoste  walitiwa hatiani kwa kosa hilo mwaka 2013 na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya jumla ya  Sh21 milioni. Walilipa faini hiyo wakaepuka kifungo.

Waliotiwa hatiani katika kesi hiyo ambao ndio wajibu maombi ya DPP ni Jackson Sifael Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saigaran ole Loitginye na Samwel Sifael Mtares.

Mbali na fedha hizo taslimu zilizoko katika akaunti za tofautitofauti Tanzania, mali nyingine ambazo DPP anaomba zitaifishwe ni nyumba, viwanja katika mikoa mbalimbali nchini ambazo  anadai zimepatikana kutokana na makosa hayo yaliyowatia hatiani katika kesi ya msingi.

Uamuzi huo wa Mahakama leo ndio utakaohitimisha mvutano mkali wa kisheria ulioibuka mahakamani siku  ya usikilizwaji maombi hayo.

Siku ya usikilizwaji maombi hayo, wakili wa wajibu maombi, Majura Magafu aliiomba Mahakama iyatupilie mbali maombi hayo akidai kuwa muombaji ameshindwa kutoa ushahidi mahakamani kuthibitisha kuwa mali hizo zote zimetokana na makosa hayo yaliyowatia hatiani.

Alidai si kila anayetiwa hatiani kwa makosa kama hayo lazima mali zake zitaifishwe na kwamba, Sheria ya Ushahidi kifungu cha 110 kiko wazi kwamba ni jukumu la kila anayeiomba Mahakama imtendee analoliomba kuithibitishia kuwa anastahili hicho anachokiomba.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro alisisitiza kuwa wajibu maombi hao walikubali katika utetezi wao kuwa Deci haikuwa na biashara nyingine isipokuwa kupokea amana za wanachama.

Magafu alidai walikubali kuwa mali nyingine zilikuwa zao binafsi na nyingine za Deci.

Aliendelea kuwa Deci haikuwa mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo na kwamba, hakuna mahali wajibu maombi walitamka kuwa hata hizo mali za Deci zilipatikana kwa njia zisizo halali na akasisitiza kuwa mjibu maombi alipaswa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha hilo.

Hata hivyo, Kimaro alidai wana ushahidi wa kutosha kwamba mali hizo walizoziorodhesha katika maombi hayo zikiwamo fedha hizo zimetokana na kosa hilo aki.

Kimaro alirejea ushahidi wa baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka na utetezi wa wajibu maombi hayo katika kesi ya msingi, ambao walidai kuwa Deci haikuwa na biashara nyingine zozote na fedha nyingine zaidi ya kupokea amana kutoka kwa wanachama.

Kwa mujibu wa ushahidi huo, Kimaro alieleza kuwa fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti ya kanisa kwa kuwa walikuwa katika mazungumzo huku akirejea utetezi wa baadhi ya wajibu maombi kuwa hawakuwa na biashara nyingine zaidi ya upatu.

Alidai wajibu maombi walishatiwa hatiani katika kesi ya jinai namba 109/2009 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kosa la kuendesha shughuli za upatu.

Kimaro alibainisha kuwa kosa hilo ni moja ya makosa makubwa na kwamba, msimamo huo ulishatolewa hata na Mahakama ya Rufani katika rufaa ya DPP kupinga uamuzi wa mahakama za chini kuwarejeshea fedha zao waliokuwa wamewekeza amana zao.

Alieleza kwua kutokana na uzito huo wa kosa, Mahakama ya Rufani pia ilielekeza DPP afungue maombi Mahakama Kuu ya kutaifisha mali zote zilizopatikana kutokana na kosa hilo.

Huku akirejea kesi mbalimbali zilizokwisha kuamuriwa na mahakama za ndani na za nje ya nchi, Kimaro alidai kuwa suala la kutaifisha mali zilizotokana na kosa la uhalifu si jipya na kwamba hata Mahakama inatunga sheria hiyo iliweka msisitizo kuwa lengo ni ili mhalifu asinufaike na uhalifu huo.

Kimaro alisisitiza kuwa hata katika kiapo chao kinzani hawajaeleza chanzo kingine cha mali hizo.

Chanzo: mwananchi.co.tz