Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatima kuachiwa mifugo 1,000 iliyokamatwa yaiva

HUKUMU Hatima kuachiwa mifugo 1,000 iliyokamatwa yaiva

Wed, 15 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imepanga Novemba 24 mwaka huu kusikiliza na kutoa uamuzi madogo juu ya kesi ya wakazi wanane wa Ngorongoro kuomba kuachiwa mifugo zaidi ya 1,000 ambayo inashikiliwa katika pori la akiba ya Pololeti Wilaya ya Ngorongoro mkoani hapa.

Katika maombi ya shauri hilo namba 106 la mwaka 2023 wanaoshitakiwa na kutakiwa kurejesha mifugo hiyo ni Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala na maofisa wa Serikali Pius Rwiza, David Mkenga, Robert Laizer na Prisca Ulomi.

Wananchi hao wa Ngorongoro waliofungua shauri hilo ni Latang Amwakindwati, Kileo Mbilika, Namuru Kitupei, Philemon Ngulumai, Nokorenta Onyia, Metiantikw Sepena na Saitoti Parmwat.

Akizungumza leo Novemba 14, Wakili wa wananchi hao, Alute Mughwai, mbele ya Jaji Nyigulila Mwaseba amesema wateja wake wamewasilisha maombi ya dharura kuomba kurejeshewa mifugo hiyo ambayo imekamatwa kinyume cha sheria.

Amesema washitakiwa hao wamekiuka amri ya Mahakama kwa kukamata mifugo hiyo licha ya Mahakama kusitishwa ukamataji wa Mifugo na watu katika eneo la Pori la Akiba Pololeti mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Hata hivyo, wakili wa washitakiwa hao watano, Kapimpiti Mugalula ameomba mahakama kuu kabla ya kutoa maamuzi apate muda wa kupitia hoja za waliopeleka shauri hilo Mahakamani.

"Mheshimiwa Jaji kwa kuwa leo ndio nimeanza kuwatetea washitakiwa naomba nipate fursa ya kupitia maombi haya ili niweze kuwasilisha hoja kinzani ndani ya siku Saba," amesema.

Wakili Mugalula amesema kwa kuwa Mifugo imeshikiliwa hifadhini kuna taratibu za kuachiwa ambazo hazipo katika Mamlaka ya wanaolalamikiwa.

Wakili Mughwai amesema wanaoshitakiwa ndio wanajua wameiweka wapi mifugo hiyo na wanaomba Mahakama kwa kuzingatia kifungu namba 68 cha sheria ya mwenendo wanashauri ya madai kutoa maamuzi ya dharura wakati bado kesi ya msingi inaendelea.

Hata hivyo, Jaji Mwaseba amesema ili aweze kutoa uamuzi ni muhimu upande wa walalamikiwa kupata fursa ya kutoa majibu kinzani.

"Hivyo Novemba 24 saa tano asubuhi tutapokea hoja kinzani katika shauri hili kabla ya kutoa uamuzi," amesema

Katika shauri jingine dogo, waleta maombi hao wanane ambao walikuwa wanawakilishwa na Mawakili Joseph Ole Shangay, Yonas Masiaya na Denis Moses waliwasilisha maombi kutaka mahakama kuomba itoe uamuzi kufatilia ofisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali kuingilia maamuzi ya Mahakama.

Katika shauri hilo, wananchi hao wameeleza Mahakamani hapo kuwa tamko la mwanasheria Mkuu wa Serikali la Oktoba 4, mwaka huu juu ya maamuzi ya Mahakama kuhusiana na uhalali wa pori la akiba la Pololeti limepotosha.

Wakili Masiaya amesema tamko hilo limetolewa kinyume cha maadili kwa sababu linapingana na maamuzi ya Mahakama ambayo ilitaka kusimama shughuli zote ndani ya pori la akiba la Pololeti hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kama Ofisi ya mwanasheria Mkuu haikubakiani na maamuzi hayo ilipaswa kukata rufaa.

"Mahakama ina wajibu wa kulinda maamuzi yake ili Umma uendelee kuna na Imani na mahakama, hivyo tunataka amri ya Mahakama kusimisha shughuli za pori la akiba kutekelezwa," amesema

Hata hivyo, Jaji Mwaseba baada ya kupokea hoja za Ofisi ya mwanasheria Mkuu wa serikali alipanga November 22 kutoa maamuzi ya shauri hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live