Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatima kesi ya kigogo IPTL leo

Seth Hatima kesi ya kigogo IPTL leo

Fri, 11 Jun 2021 Chanzo: ippmedia.com

Mshtakiwa, Seth alifikishwa kwa dharura katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili wa Serikali, Martenus Marando, akiiwakilisha Jamhuri alidai mshtakiwa aliandika barua mbalimbali kupitia mawakili wake kwa lengo la kufanya mazungumzo ya kumaliza shauri hilo.

"Jamhuri tumeona ni vyema kuja mbele ya Mahakama hii kuomba kukutana na mshtakiwa mbele ya mawakili wake tuweze kuzungumza naye kupata ufafanuzi wa barua zake na kile alichodhamiria kwa dhati kifanyike," alieleza Marando.

Alidai ombi lao lilikuwa hilo na endapo upande wa utetezi hautakuwa na pingamizi, waliomba mshtakiwa apelekwe mahakamani leo.

Upande wa utetezi haukuwa na pingamizi.

Wakili Marando alidai kwa vile upande huo hauna pingamizi aliomba mshtakiwa apelekwe mahakamani leo ili upande wa Jamhuri uwasilishe mrejesho wa kile walichozungumza.

Mahakama ilikubali ombi hilo na kuahirisha kesi hadi leo, na kuamuru mshtakiwa apelekwe mahakamani.

Mshtakiwa alipaswa kufika mahakamani Juni 17, mwaka huu, tarehe ambayo ilipangwa na mahakama Juni 3 wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Awali Juni 3, mwaka huu, upande wa Jamhuri ulidai mahakamani kwamba kesi hiyo ya uhujumu uchumi inasubiri mwongozo wa Mkurugenzi mpya wa Mashtaka (DPP), ili kumaliza mazungumzo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa na kujua hatua iliyofikia katika mazungumzo hayo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai mazunguzo yaliyokuwa yakifanyika kwa ajili ya kumaliza kesi dhidi ya mshtakiwa Seth yanaendelea pale yalipoishia, wanasubiri mwongozo kutoka kwa DPP mpya aliyeteuliwa hivi karibuni.

Seth na Wakili Joseph Makandege waliwasilisha ombi kwa DPP wakionyesha nia yao ya kutaka kumaliza kesi kwa kukiri makosa yao, lakini, Mei 6, mwaka huu, Wakili Makandege aliondoa nia yake ya kufanya mazungumzo na DPP, akieleza kwamba mazungumzo hayo hayana afya na yamechukua muda mrefu kukamilika.

Mbali na Seth, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara James Rugemalira na wakili Makandege. 

Rugemarila, ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, wanadaiwa kutenda makosa hayo katika Jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwamo ya utakatishaji fedha, miongoni mwa mashtaka hayo yapo ya kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Chanzo: ippmedia.com