Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hati ya wito kwa wajibu rufaa wenzake Sabaya kutolewa mara ya tatu

Sabaya Pic2 Data Hati ya wito kwa wajibu rufaa wenzake Sabaya kutolewa mara ya tatu

Wed, 28 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imeagiza kutolewa hati ya wito wa mahakama kwa mara ya tatu kwa wajibu rufaa wawili katika rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kupinga hukumu iliyomwachia huru aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake.

Rufaa hiyo namba 155/2022, inapinga hukumu iliyowaachia huru Ole Sabaya na wenzake waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ambapo mbali na Sabaya wajibu rufaa wengine ni Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Akiahirisha rufaa hiyo leo Jumatano, Desemba 28,2022, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Fadhil Mbelwa, amesema kwa kuwa matangazo ya hati ya wito mahakamani yameshatolewa mara mbili, yatatolewa kwa mara ya tatu ili wajibu rufaa wawili ambao ni Macha na Msuya waweze kufika mahakamani na shauri hilo kuendelea na usikilizwaji.

Amesema baada ya tangazo hilo kutolewa kwa mara ya tatu katika magazeti ya Mwananchi na The Citizen kama yalivyotolewa ya awali, rufaa hiyo itasikilizwa Januari 17,2023 na kabla ya kusikilizwa tarehe hiyo itatajwa Januari 9, 2023.

Mbali na Sabaya ambaye leo aliwakilishwa na wakili Fauzia Mustafa, mjibu rufaa mwingine ambaye alikuwepo mahakamani hapo ni Mnkeni, huku mjibu rufaa wa tatu (Aweyo) ambaye hakuwepo mahakamani hapo akiwakilishwa na wakili Fridolin Bwemelo.

Wakili Bwemelo kwa niaba ya mteja wake aliomba kupatiwa mwenendo, hukumu na nakala za vielelezo vilivyotolewa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ili waweze kujiandaa kwa ajili ya usikilizwaji kwa tarehe husika.

Naye wakili Fauzia aliomba kupatiwa nakala ya vielelezo vilivyotolewa katika kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,hati ya mashitaka ya kwanza pamoja na hati ya pili iliyofanyiwa marekebisho.

"Mheshiwa Hakimu nimepata taarifa kwenye gazeti la Desemba 21, nilikuwa naomba nipatiwe mwenendo wa kesi,nakala ya hukumu,vielelezo vilivyotolewa wakati wa usikilizwaji wa shauri,sababu za rufaa ili niweze kuona namna natafuta wakili atakayeniwakilisha,"aliomba Mnkeni

Wakili wa Serikali mwandamizi, Akisa Mhando, anayemwakilisha muomba rufaa,aliiomba mahakama kutaja shauri hilo Januari 9,2023 kabla ya tarehe ya kusikilizwa ili kuona endapo tangazo limetolewa na wahusika wamelipata.

"Nakala zitolewe kwa wajibu rufaa ili waweze kujiandaa kama walivyoomba na tarehe ya usikilizwaji ni Januari 17, 2023 kama ilivyopangwa ila itatajwa Januari 9,"alisema Hakimu

Awali, Desemba 21, 2022 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha,Judith Kamala alisema rufaa hiyo itaendelea kusikilizwa leo baada ya tangazo la hati ya wito kwa wajibu maombi wanne kutolewa kwa mara ya pili katika magazeti baada ya kuamriwa na Jaji Salma Maghimbi aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo.

Rufaa hiyo inapinga hukumu iliyotolewa Juni 10, 2022 na Hakimu Mkazi Patricia Kisinda wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, hukumu iliyowaachia Sabaya na wenzake sita waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2021 katika mahakama hiyo ya chini. Mwananchi. Fikiri Tofauti.

Chanzo: Mwananchi