Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Halima Mdee ashikiliwa kituo cha polisi Oysterbay

84598 Pic+mdee Halima Mdee ashikiliwa kituo cha polisi Oysterbay

Mon, 18 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Wilaya ya Kinondoni linamshikilia mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ambaye jana Ijumaa Novemba 15, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliagiza akamatwe pamoja na wabunge wengine watatu wa chama hicho.

Wabunge wengine ambao mahakama hiyo iliagiza wakamatwe kutokana na kukiuka masharti ya dhamana ni John Heche (Tarime Vijijini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Ester Bulaya (Bunda).

Halima ameripoti kituo cha polisi Oysterbay leo Jumamosi Novemba 16, 2019 kuitikia amri ya mahakama lakini alizuiwa kutoka.

Amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya wabunge hao kutokuwepo mahakamani bila taarifa yoyote. Hata wadhamini wao pia hawakuwepo. Pia, Hakimu Simba alitoa hati ya wito wa wadhamini wa wabunge hao kujua sababu za kutowapeleka washtakiwa mahakamani.

Kabla ya kutoa amri hizo, Hakimu Simba alisema jana kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa, washtakiwa wengine waliwahi, lakini wabunge hao wanne hadi saa 4:05 asubuhi walikuwa hawajafika mahakamani bila sababu za msingi.

Akizungumza na Mwananchi leo kamanda wa polisi wilayani humo, Musa Taibu amesema Halima atafikishwa mahakamani Jumatatu Novemba 18, 2019.

“Kama mahakama zingekuwa wazi tungempeleka lakini leo ni Jumamosi hatuwezi, tunaendelea kumshikilia kwa kuwa ni amri ya mahakama,” amesema Taibu.

Mdee na viongozi wengine wanane wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.

Wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji  na manaibu katibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).

Chanzo: mwananchi.co.tz