Dar es Salaam. Halima Mdee, mshtakiwa wa saba katika kesi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa hakuwahi kushiriki maandamano.
Mbunge huyo wa Kawe ameeleza hayo leo Alhamisi Desemba 5, 2019 wakati akitoa ushahidi katika kesi ya jinai namba 112/2018 yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi inayomkabili pamoja na wenzake.
Mdee akiongozwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai kuwa Februari 16, 2018 kabla ya mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa marudio jimbo la kinondoni alikuwa bungeni Dodoma.
Amedai kuwa siku hiyo afya yake haikuwa nzuri na alishiriki mkutano huo kuonyesha mshikamano na upendo kwa mgombea na baada ya kushuka jukwaani aliondoka.
"Nilifika Dar es Salaam saa 5 asubuhi na kwenda kwenye mkutano saa tisa alasiri. Baada ya kuhutubia niliondoka kwa kuwa nilikuwa naenda kujiandaa na safari,” amesema Halima.
Akijitetea mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, mbunge huyo amesema alikamatwa na askari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiwa anatokea Afrika Kusini kwenye matibabu.
Alipoulizwa na Kibatala maneno aliyozungumza jukwaani yalikuwa yana dhana gani, alijibu alikuwa akimuombea kura mgombea ubunge, Salum Mwalimu.
Akizungumzia maneno aliyotamka jukwaani amesema alieleza changamoto mbalimbali kama kufukuzwa bungeni, watu kupotea na wafanyabiashara kufilisiwa.