Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hali Ilivyokuwa siku Polisi walivyobebeshwa madai ya kifo cha mtuhumiwa

50049 MADAI+PIC

Wed, 3 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni saa saba mchana wa Machi 24, 2019 napokea ujumbe kwenye simu yangu ya mkononi ukinitaarifu tukio linalodai kuna mwananchi amepigwa na polisi na kusababisha kifo chake.

Kama mwandishi naona hii ni “tip” (wazo la habari), naanza safari ya kuutafuta undani wa habari hii. Ni umbali wa zaidi ya kilomita 60 kutoka Geita mjini kwenda katika Kijiji cha Nyakafuro, kata ya Chigunga wilayani Geita.

Saa tisa alasiri nawasili kijijini hapo, nakutana na umati wa watu katika eneo la uwanja ambao hutumika kama soko, lakini kwa siku hiyo wananchi hawakuwa sokoni bali walikuwa wakidai haki.

Naanza kuzungumza na baadhi yao wanaoonekana mioyo yao imejaa hasira kutokana na kauli walizokuwa wakizitoa si kutokana na kifo cha mwenzao, Jackson Charles bali lawama nyingi kwa polisi hasa wa kituo cha Butundwe.

Pascal Charles ambaye ni kaka wa marehemu (Jackson Charles) anasema licha ya wao kutoka na mwili hospitali, lakini walipofika uwanjani hapo walikutana na wananchi na kuzuia mwili hadi wajue sababu za kifo hicho.

Anasema wao kama familia hawana sababu ya kwenda kinyume na matakwa ya jamii wanayoishi nayo kwa madai vitendo vya polisi kutumia nguvu vimezidi kwani wamekuwa wakipigwa mara kwa mara.

Uamuzi wa wananchi unakubaliwa na familia na kuamua kukataa kuupokea mwili wa ndugu yao licha ya kutoka nao Hospitali ya Mkoa wa Geita walikosaidiwa jeneza na gari la kubeba mwili lililotolewa na polisi wilayani humo. Wananchi hao walisema hawapo tayari kuzika hadi pale watakaposikilizwa na Serikali na polisi waliopo kituoni hapo kuondolewa.

Wakati wananchi wakidai ndugu yao amefariki kutokana na kipigo cha polisi, jeshi hilo lilisema mwananchi huyo alipoteza maisha baada ya kuugua akiwa mahabusu na kuwa taarifa za kitabibu zinaonyesha alikuwa na malaria kali na kifafa.

Maiti yarudishwa hospitali

Baada ya dereva kuzunguka na mwili zaidi ya mara tatu akienda kituo cha polisi na kurudi katika uwanja huo, mwishowe wakaurudisha mwili Hospitali ya Geita.

Mwili huo umekaa kwenye chumba cha maiti kwa siku mbili hadi pale mkuu wa wilaya ya Geita alipoingilia kati kutafuta suluhu ili wananchi waridhie kumpa heshima ya mwisho Jacson kwa kumsitiri kwenye nyumba yake ya milele.

Jeshi la polisi

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Mponjoli Mwabulambo anasema mtuhumiwa huyo alikamatwa akituhumiwa kujihusisha na mapenzi na mwanafunzi.

Akizungumzia malalamiko ya mtuhumiwa huyo kupigwa akiwa mahabusu, Kamanda Mwabulambo alikana askari wake kuhusika na kusisitiza mtuhumiwa aliugua malaria kali na kifafa.

Mkuu wa wilaya afika kijijini

Machi 26, saa 10 alasiri Mkuu wa wilaya ya Geita, Josephat Maganga akiwa na kamati ya ulinzi na usalama wakiwa na mwili wa Jackson walifika katika kijiji hicho na kukuta umati wa wananchi ukiwasubiri.

Akizungumza na wananchi hao mkuu wa wilaya alisema hiyo ni mara ya tatu kufika katika kijiji hicho na mara zote hufika hapo kutokana na malalamiko kati ya wananchi na polisi.

Anasema Serikali haijaagiza mtu yeyote apigwe na mtumishi atakayeshindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi atachukuliwa hatua. Aliwaomba wananchi wampe muda ili jambo hilo lifanyiwe uchunguzi.

Anasema kituo cha polisi Butundwe kina askari wanne ambao si rahisi kuwahudumia wananchi wote wakaridhika na utendaji kazi wao na kusema anachokiona sasa imani kati ya wananchi na polisi hao sasa haipo.

Mkuu huyo wa wilaya anasema kabla ya kufikwa na mauti Jackson alikamatwa akituhumiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Chigunga na kwa taarifa alizopewa aliugua malaria maelezo ambayo wananchi waliyapinga.

Baba wa Marehemu aeleza

Charles Sengema ambaye ni baba mzazi wa marehemu Jackson anasema tangu mwanaye azaliwe miaka 24 iliyopita, hajawahi kuugua ugonjwa wa kifafa, hivyo si vyema kunasibishwa na ugonjwa huo hata kidogo.

Sengerema anadai mtoto wake alikamatwa na polisi na kupigwa mbele ya wananchi kisha walimpeleka kituo cha polisi na baadaye alizidiwa na kupelekwa kituo cha afya Chikobe ambako siku iliyofuata (Machi 22) alipewa rufaa ya kwenda hospitali ya mkoa wa Geita.

Mzee huyo anasema licha ya mwanaye kuwa hospitali huku akiwa mahututi aliendelea kuwa chini ya ulinzi wa polisi pingu zikiwa mikononi mwake.

Anasema baada ya kufariki dunia alitaka uchunguzi ufanyike na kwamba baada ya mwili kukaguliwa ulibainika kuwa na majeraha makubwa mgongoni huku ukikutwa na shimo kwenye eneo la shingo.

Hata hivyo, licha ya baba kuridhia kumzika mtoto wake bado ilishindikana kwa kuwa hakuwa na shamba hadi pale Serikali ya kijiji ilipoagizwa na mkuu wa wilaya kutoa ardhi kwa ajili ya maziko.

Uhusiano wa polisi na wananchi

Wakizungumza mbele ya mkuu wa wilaya wananchi wa kijiji hicho walidai polisi wa kituo cha Butundwe wamekuwa wakiyafanya matatizo ya wananchi kuwa mtaji ambapo mtu anayebainika kumpa mimba mwanafunzi kesi humalizwa kwa mtuhumiwa kulipa kati ya Sh1 milioni hadi Sh2 milioni.

Mmoja wa wananchi aliyekataa kutajwa jina gazetini, anasema yeye ni miongoni mwa waliowahi kubambikiwa kesi akidaiwa kutaka kukichoma moto kituo cha polisi, unyang’anyi wa kutumia silaha lakini askari walishindwa kuthibitisha madai yao kwa ushahidi.

Yohana Kasheku na Yohana Madirisha wanadai polisi wamekuwa wakivamia nyumba zao na kuwapiga bila ya kuangalia wanayemfanyia hivyo ama ni mwanammke au mwananume. Hivyo wamechoshwa na vitendo hivyo, wanachotaka ni askari wa kituo hicho wote waondolewe.



Chanzo: mwananchi.co.tz