Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu, mwenyekiti halmashauri Chato washitakiwa kwa rushwa

38703 Chato Hakimu, mwenyekiti halmashauri Chato washitakiwa kwa rushwa

Tue, 29 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita, Batholomeo Manunga na hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya hiyo, Yohana Myombo wameburuzwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa makosa ya kutoa na kupokea rushwa.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kaimu ofisa mkuu wa Takukuru mkoani Geita, Mwamba Masanja leo Jumapili Januari 27, 2019 imeeleza kuwa washtakiwa hao walipandishwa mahakamani juzi Ijumaa.

Masanja amesema makosa hayo ni kinyume na kifungu cha 25(1) (a), (b) na (2) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Alisema kesi hiyo ya jinai namba 42/2019 ilisomwa na mwendesha mashtaka wa Takukuru, Dennis Lekayo mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Jovith Kato.

Akielezea mashitaka hayo mahakamani, Lekayo alisema Desemba 11, 2018 mshtakiwa wa kwanza Batholomeo Manunga ambaye ni diwani wa Bwongera alikuwa anakabiliwa na tuhuma za uvuvi haramu ambazo zingempelekea kufikishwa mahakamani lakini alitoa rushwa kwa hakimu Yohana Myombo ili kutengeneza mazingira ya kusaidiwa pindi atakapofikishwa mahakamani hapo.

Alidai siku moja baadaye mshtakiwa wa kwanza alifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya kesi ya uvuvi haramu katika wilaya ya Chato.

Mwendesha mashtaka alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa Batholomeo akiwa wilayani Geita alituma Sh4 milioni kwenda kwenye namba ya wakala wa M-Pesa aitwae Keziah Mayenga ambazo mshtakiwa wa pili Yohana Myombo alimwagiza karani wake kwenda kuchukua fedha hizo kwa wakala.

Washtakiwa wamekana makosa hayo na wako nje kwa dhamana baada ya kukidhi vigezo vya kuwa na wadhamini wawili wakuaminika waliosaini fungu la dhamana la Sh2 milioni na kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 28 itakapokuja kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.



Chanzo: mwananchi.co.tz