Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu kesi ya akina Tenga atoa siku 14 upelelezi ukamilike

39516 Tengapic Hakimu kesi ya akina Tenga atoa siku 14 upelelezi ukamilike

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ameutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi ndani ya siku 14 katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa kampuni ya mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwemo wakili,  Dk Ringo Tenga.

Hakimu Simba ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari Mosi, 2019 baada ya wakili wa Serikali, Simon Wankyo kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika.

“Bado tunafuatilia kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) na tupo kwenye hatua za mwisho hivyo kesi itakapokuja tena tutakuwa tumekamilisha hizo hatua," amedai Wankyo.

Hakimu Simba amesema upande wa mashtaka wamekuwa wakisema wapo kwenye hatua za mwisho kukamilisha upelelezi na wameshaongea hivyo zaidi ya mara 40 hakuna majibu wanayoleta.

"Natoa msisitizo, hayo maneno ya kufikia hatua za mwisho mmeshaongea  zaidi ya 40 na tumeshafika Februari hakikisheni ndani ya siku 14 kesi hii itakapokuja tena muwe mmeshakamilisha,” amesema Simba.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mhandisi, Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo; mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni; mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha na kampuni ya Six Telecoms.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama hiyo Novemba 20, 2017 kujibu mashtaka sita yakiwemo ya utakatishaji fedha.

Katika kesi ya msingi, Dk Ringo ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanadaiwa kuwa kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14, 2016 Dar es Salaam walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa  chini ya kiwango cha Dola 0.25 za Marekani kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia,  katika kipindi hicho wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola 3,282,741.12 za Marekani kwa TCRA kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao wanadaiwa  katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola 466,010.07 za Marekani  kwa TCRA.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Hafidhi, Noni, Tenga na Chacha wanadaiwa kuwa walitumia ama walisimamia Dola 3,282,741.12 za Marekani wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashitaka yaliyotangulia.

Washitakiwa hao  wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola 3,748,751.22 za Marekani (zaidi ya Sh8 bilioni ).

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 15, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana baadhi ya mashtaka kutokuwa na dhamana.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz