Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu kesi ya akina Mbowe awashukia wanaompigia simu

9872 Pic+mbowe TanzaniaWeb

Fri, 3 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri amewaonya wanaompigia simu wakati akiwa nyumbani kwake, huku akisema huo si ustaarabu.

Hakimu Mashauri anayesikiliza kesi inayowakabili viongozi wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alitoa kauli hiyo jana wakati akisikiliza shauri hilo ambalo liliahirishwa hadi Agosti 6 kutokana na mshtakiwa wa tano, Esther Matiko kutofika mahakamani.

Bila kuwataja majina watu wanaompigia simu, alisema akiwa kazini anakuwa hakimu na akiwa nyumbani anakuwa Mashauri.

“Nikiwa nyumbani ni Mashauri na nikiwa kazini ni hakimu, hivyo wanaonipigia simu nikiwa nyumbani huo sio utaratibu,” alisema.

Jana, Mahakama hiyo ilishindwa kuwasomea maelezo ya awali viongozi hao wa Chadema kutokana na Matiko kutofika mahakamani.

Akitoa udhuru wa mshtakiwa huyo, wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala aliieleza mahakama kuwa Matiko amepigiwa simu ya dharura kutoka katika shule anayosoma mwanaye mjini Nairobi, Kenya na kulazimika kwenda.

Hakimu Mashauri alimhoji mdhamini wa mbunge huyo wa Tarime Mjini juu ya sababu za mshtakiwa huyo kwenda Nairobi na kujibiwa kuwa hata yeye hafahamu zaidi ya Matiko kumweleza kuwa anakwenda shule anayosoma mwanaye.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi ulimlaumu mdhamini huyo kwa kutojua sababu ya kilichompeleka mbunge huyo Nairobi na kutaka akirejea awe na uthibitisho.

“Upande wa mashtaka hatuna la kufanya ila kesi itakapotajwa inabidi aieleze Mahakama pamoja na uthibitisho wa nini alichoitiwa huko,” alisema Nchimbi.

Aliiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6, huku Kibatala akiomba ipangwe Agosti 13 kwa kuwa Agosti 6 atakuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu. Hata hivyo, Hakimu Mashauri alikubaliana na ombi la upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Wengine ni katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Matiko.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 12 ikiwamo kuchochea ghasia, kukaidi amri ya polisi, uchochezi na uasi.

Wanadaiwa kufanya makosa hayo Februari 16, wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Katika tukio hilo, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini alipigwa risasi akiwa kwenye daladala, eneo la Mkwajuni.

Chanzo: mwananchi.co.tz