Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu awatolea uvivu Polisi wanaozuia wanahabari kesi ya mauaji Mtwara

Mauaji Polisi Mtwara Hakimu awatolea uvivu Polisi wanaozuia wanahabari kesi ya mauaji Mtwara

Tue, 8 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara leo Machi 8, 2022 imewataka askari polisi kuwaacha wanahabari kufanya majukumu yao wakati kesi ya maafisa saba wa polisi wanaoshtakiwa kwa mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Musa Hamis ikiendelea mahakamani hapo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Lugano Kasebele amesema leo mahakamani hapa kabla hajaanza kusikiliza kesi hiyo ambayo iko katika hatua ya kutajwa.

"Kuna jambo kidogo ningependa kulizungumza, nimepokea malalamiko kutoka kwa wanahabari kwamba wanakatazwa kuingia ndani kusikia na kuona kinachoendelea wakati kesi inaendelea.

"Naomba niseme kwamba, hii ni mahakama ya wazi anaruhusiwa mtu yoyote kuingia na kushuhudia yanayoendelea. Wanahabari wana haki kama raia wengine wowote kuingia na kusikiliza,” amesema Hakimu Kasebelele.

Amesema kikubwa ambacho wanahabari hawaruhusiwi ni kupiga picha kurekodi wakati mahakama inaendelea.

“Waingie ila masharti na vigezo vyote vizingatiwe," amesema Kasebele.

Kauli ya Hakimu huyo inatokana na hatua ya maofisa wa polisi kuwazuia na kuwabugudhi kwa maneno na vitendo wanahabari wakiwemo wapiga picha wanaofika mahakamani hapo kutekeleza wajibu wao, likiwemo tukio la Februari 22, 2022 ambapo mwanahabari walizuiwa kabisa kutekeleza wajibu wao.

Hata hivyo, leo ambapo kesi hiyo imetajwa tena mahakamani hapa wanahabari waliruhusiwa kuingia kusikiliza kesi hiyo na kupiga picha kabla kesi haijaanza huku mshtakiwa mmoja akiwa amejifunika na taulo, wengine wakiinama na wengine barakoa.

Kesi hiyo inawakabili maafisa saba wa polisi ambao ni Ofisa upelelezi (OC CID) wilaya ya Mtwara ambaye ndie mshtakiwa namba moja, Gilbert Kalanje, Mkuu wa Kituo cha polisi Mtwara, (OCS), Charles Onyango, Ofisa wa intelijensia ya jinai mkoa wa Mtwara, Charles Kisinza na Mkaguzi wa Polisi, John Msuya pamoja na Mganga Mkuu wa zahanati ya polisi, Marco Mbuta.

Wengine ni Mkaguzi wa polisi, Shirazi Mkupa na Koplo Salum Juma Mbalu.

Aidha Mahakama hiyo imeahirisha kesi hiyo hadi Machi 22, 2022 itakapotajwa tena kwa kilichoelezwa na Hakimu Kasebele kuwa upelelezi haujakamilika.

Akielezea hatua ya kesi mahakamani hapo Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Severine Mganga amesema upelelezi haujakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kesi hiyo kutajwa.

Wastakiwa wote walifika mahakamani majira ya saa 2.44 asubuhi wakiwa chini ya ulinzi mkali.

Maofisa saba wa Jeshi la Polisi, wanashikiliwa na jeshi hilo mkoani Mtwara kwa tuhuma za kumpora mfanyabiashara mmoja wa madini Sh70 milioni na kisha kudaiwa kumuua kwa kumchoma kwa sindano ya sumu na kuutupa mwili wake baharini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live