Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema upande wa mashtaka wasipokamilisha upelelezi wa kesi inayowakabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA), Madeni Kipande na wenzake atawarudisha polisi au Takukuru.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh4.2 bilioni.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali, Mosie Kaima kuieleza mahakana hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilka.
Ndipo Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira alisema shauri hilo kama halijakamilika tarehe ijayo washtakiwa hao atawarudisha polisi au Takukuru
"Upande wa mashtaka mwende mkaamue cha kufanya tarehe ijayo kama shauri hili halijakamilika washtakiwa nitawarudisha Polisi au Takukuru,"alisema Rugemarila.
Hakimu Rugemalira aliahirisha shauri hilo hadi June 15, 2023 litakapokuja kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana.
Mbali na Kipande washtakiwa wengine wengine ni Peter Gawile (58) Ofisa Rasilimali Watu wa TPA, Casmily Lujegi (65) Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA, Mashaka Kisanta (59) Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi na Kilian Chale (51) Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Mkazi wa Mbezi Makabe.
Inadaiwa kati ya Oktoba Mosi,2014 na Oktoba Mosi 2020 jijini Dar es Salaam, walikula njama na kuisababishia TPA hasara ya Sh 4.2 bilioni.
Inadaiwa washtakiwa hao walitangaza zabuni hiyo, bila kupata kibali cha Bodi ya zabuni ya mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni za zabuni hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo jambo lililosababisha TPA hasara ya Dola za Marekani milioni 1.8 Sawa na zaidi ya Sh 4.2 bilioni.