Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu atoa siku 14 upelelezi kesi ya Dk Tenga ukamilike

Fri, 22 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba ametoa siku 14 kwa upande wa mashtaka kuhakikisha wanakamilisha upelelezi  katika kesi inayowakabili vigogo wa Six Telecoms akiwemo wakili Dk Ringo Tenga.

Hatua hiyo imekuja baada ya wakili wa Serikali, Batilda Mushi kuieleza mahakama hiyo kuwa jalada bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) linafanyiwa kazi wapo kwenye hatua za mwisho kukamilisha upelelezi.

"Mheshimiwa shauri hili limekuja kwa ajili ya kutajwa upelelezi upo kwenye hatua ya mwisho kukamilika bado haujakamilika tunaomba tarehe nyingine ,"alidai Batilda.

Hakimu Simba alisema upande wa mashtaka hakikisheni mnakamilisha upelelezi wa kesi hiyo ili shauri hilo liweze kuendelea siku itakapokuja tena mahakamani hapo.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Aprili 5, 2019 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Washtakiwa wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni wa hiyo, Peter Noni, mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha na kampuni ya Six Telecoms.

Mahakama yataka maelezo ya mashahidi kesi ya akina Dk Tenga

Katika kesi ya msingi, Dk Tenga ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanadaiwa kuwa, kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14,2016 maeneo ya Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini(TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao , wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shitaka la utakatishaji fedha, Hafidhi, Noni,Tenga na Chacha, wanadaiwa kuwa walitumia ama walisimamia Dola za Marekani 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashitaka yaliyotangulia.

Vile vile ,washitakiwa hao wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22 (sawa na Sh. 8bilioni ).



Chanzo: mwananchi.co.tz