Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu atoa masharti upande wa mashtaka kesi ya Michael Wambura

49134 Tffpic

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu umeutaka upande wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura, kila shauri hilo linapotajwa kueleza ni hatua upelelezi ulipofikia.

Wambura anakabiliwa na mashtaka 17 yakiwamo ya kutakatisha zaidi ya Sh100 milioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2019.

Hatua hiyo imekuja baada ya wakili wa Serikali Elizabeth Mkunda, kuieleza  mahakama hiyo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na wanafuatilia ili kujua upelelezi ulipofikia.

"Upelelezi haujakamilika tunaendelea kufuatilia umefikia wapi hivyo naiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," alidai Mkunda.

Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo  Kelvin Mhina, alisema upande wa mashtaka kila wanapokuja kwenye shauri hilo waieleze mahakama hiyo hatua upelelezi ulipofikia.

"Lengo ni kuhakikisha upelelezi unakamilika hivyo kila mnapokuja mnatwambia ipo kwenye hatua gani," alidai Mhina.

Mahakama hiyo iliahirisha shauri hilo hadi Aprili 11,2019 itakapotajwa tena na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Katika mashtaka hayo 17; moja ni la kughushi, moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004 katika sehemu isiyojulikana jijini Dar es Salaam.

Siku hiyo, Wambura kwa nia ya kutapeli  anadaiwa kutengeneza barua ya kughushi ambayo haina kumbukumbu namba akionyesha imeandikwa na E Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa  Kampuni ya Jeck system, anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa Dola 30,000 za Marekani na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka la kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, mshtakiwa alitoa barua iliyokuwa haina kumbukumbu namba  ya Julai 6, 2004, akijifanya ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa Dola 30,000 za Marekani  na riba waliyokopeshwa TFF huku akijua  siyo kweli.

 

Kuanzia shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia zaidi Sh95 milioni kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa ni sehemu ya malipo ya jumla ya  fedha mbalimbali na riba kutoka kwa kampuni ya Jeck System Ltd, huku akijua siyo kweli.

Pia, katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 17, 2015 katika ofisi za TFF, kwa njia ya udanganyifu mshtakiwa alijipatia Sh10 milioni kutoka TFF kwa kuonyesha kuwa ni malipo ya Dola 30,000 za Marekani  na riba kutoka kampuni hiyo ya Jeck jambo ambalo siyo kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadaiwa kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014 makao makuu ya shirikisho hilo,  alijipatia Sh25 milioni  kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia, shtaka jingine utakatishaji fedha haramu, mshtakiwa anadaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21, 2015 alijipatia Sh75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali na zimetokana na   kughushi.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz