Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu atishia kuifuta kesi ya aliyekuwa mhasibu Takukuru

59307 Gugaipic

Thu, 23 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema itaifuta kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato halali inayomkabili aliyekuwa  mhasibu mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na mwenzake.

Imesema itachukua uamuzi huo iwapo upande wa mashtaka watashindwa kuleta mashahidi kwa wakati kama walivyokubaliana.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Mei 23, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kudai hawana shahidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi.

"Nyie upande wa mashtaka kama mnaona kuna mtu anakwamisha kuleta mashahidi mahakamani  mtuambie ili mahakama ishughulike naye.”

"Kwa sababu hii ni kesi ya muda mrefu kama mtashindwa kuleta mashahidi wa kutosha kama mlivyoahidi nitaifuta hii kesi,” amesema hakimu Simba.

Amesema haoni sababu ya kesi kuendelea kuahirishwa wakati jukumu la upande wa mashtaka ni kuhakikisha wanaleta mashahidi wa kutosha kwa sababu kesi hiyo inasikilizwa mfululizo.

Pia Soma

"Leteni mashahidi wa kutosha ili kesi hii iweze kuisha na washtakiwa wajue hatima zao. Kama ma wanafungwa wafungwe kwa wakati na kama wanaachiwa waachiwe," amesema Hakimu Simba.

Awali, wakili wa Takukuru, Lupyana Mwakatobe amedai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini mashahidi waliopaswa kutoa ushahidi wamechelewa kupata barua za wito wa mahakama.

Baada ya maelezo hayo, wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa alitaka kujua mashahidi hao waliopelekewa barua za wito  wanatoka wapi na majina yao.

Akijibu hoja hiyo, Mwakatobe amedai kuwa upande wa mashtaka ulipeleka barua za wito wa mahakama kwa Msajili wa Ardhi Kanda ya Mwanza na kwa Ofisa Ardhi Mteule katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 3, 2019, itakapoendelea na ushahidi.

Washtakiwa  wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Tayari mashahidi 13 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya Gugai.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake, wanakabiliwa na makosa 43;  19 kati ya hayo  ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali.

Pia, Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake akidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

Inadaiwa kuwa akiwa jijini Dar es Salaam kama mwajiriwa wa Takukuru alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni ambazo hazilingani na kipato chake cha awali na cha sasa, huku akishindwa kuzitolea maelezo.

Chanzo: mwananchi.co.tz