Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu ataka kesi ya Mo Dewji kuendelea bila washtakiwa wengine

94438 Dewji+pic Hakimu ataka kesi ya Mo Dewji kuendelea bila washtakiwa wengine

Wed, 5 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu nchini Tanzania imetaka kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili dereva taxi, Mousa Twaleb kuendelea bila washtakiwa wengine ambao hawajakamatwa.

Twaleb  anakabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kumteka nyara mfanyabiashara maarufu Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Februari 4, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakamani hiyo, Huruma Shaidi wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Alieleza hayo baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

"Kwa nini mshtakiwa huyu asishtakiwe peke yake ili upelelezi wa kesi ukamilike  kwa wakati kuliko kuendelea kusubiri washtakiwa wengine ambao bado hawajakamatwa?”

"Hapa upelelezi unachelewa kukamilika kutokana na washtakiwa wengine ambao bado hawajakamatwa. Kwa nini asishtakiwe yeye ili kesi iendelee halafu hao wengine wakikamatwa watakuja kuunganishwa naye, au nyie mnasemaje upande wa mashtaka,"  amehoji hakimu huyo.

Pia Soma

Advertisement
Hakimu Shaidi baada ya kutoa maelezo hayo, wakili wa upande wa mashtaka, Tulli Helela amedai maelezo hayo ameyapokea na atayapeleka kwa bosi wake kwa ajili ya uamuzi.

Awali, Wakili Helela alieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja ya upande wa mashtaka, ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 18, 2020.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mbali na Twaleb, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 42/2019 ni raia wa Afrika Kusini, Phila Tshabalala na wengine wanne ambao ni raia wa Msumbiji, Henrique Simbue, Daniel Berdardo, Issac Tomu na Zacarious Junior.

Katika kesi ya msingi wanadaiwa kutenda makosa hayo kati  ya Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Johannesburg, nchini  Afrika Kusini.

Wanadaiwa kwa makusudi walitoa msaada wa kutendeka vitendo vya jinai na uhalifu wa kupangwa kwa lengo la kujipatia faida.

Imedaiwa kuwa Oktoba 11, 2018 katika maeneo ya Hoteli ya Colloseum  wilayani Kinondoni, Twaleb na wenzake  walimteka nyara Dewji kwa nia ya kumhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Julai 10, 2018 katika maeneo ya Mbezi Beach wilaya ya  Kinondoni, Twaleb na wenzake walitakatisha Sh8 milioni wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz