Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu ashindwa kutoa uamuzi kesi ya vigogo Rahco

Sat, 16 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kutoa  uamuzi katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili  vigogo wa  Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco) kutokana na Hakimu kutokamilisha kundaa uamuzi huo.

Mahakama hiyo ilipanga kutoa uamuzi huo leo Ijumaa Februari 15, 2019 wa kuwafutia mashtaka au kutowafutia mashtaka vigogo hao, wanaokabiliwa na mashtaka manane likiwemo la kuisababishia Serikali, hasara ya Dola 527,540.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amedai kuwa alipanga kutoa uamuzi huo leo lakini anahitaji kuahirisha kwa muda kwa ajili ya kumpa muda wa kumaliza kuandaa uamuzi huo.

"Tukubaliane, nahitaji muda kidogo wa kumalizia kuandika uamuzi tufanye ahirisho fupi kwa ajili ya kumalizia kuandika uamuzi," alidai Hakimu Simba.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 19 mwaka huu atakapotolea uamuzi wa kesi hiyo.

Januari 24, mwaka huu, upande wa utetezi uliwasilisha ombi la kuifuta kesi hiyo na kuwaachia huru washitakiwa hao kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kukamilisha upelelezi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Rahco, Benhardard Tito; mwanasheria wa zamani wa kampuni hiyo, Emmanuel Massawe na mwakilishi wa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma.

Washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande takribani miaka miwili na miezi 12 sasa, kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Tito na wenzake walifikishwa kwa mara  ya kwanza, Mahakama ya Kisutu  Machi 14, 2016 kujibu mashtaka manane likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi, 2014 na Septemba 30, 2015 kwa nia ya kutenda kosa walikula njama kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Tito, anadaiwa kuwa Februari 27, 2015 katika ofisi za Rahco zilizopo Ilala alitumia madaraka yake vibaya kwa kuiajiri Kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Ltd kama mshauri wa mradi wa uimarishaji wa reli ya kati, bila idhini ya Bodi ya Rahco.



Chanzo: mwananchi.co.tz