Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu aona hoja Sabaya, wenzake kujua hatma yao

Bfcae21c6c24ef73c834ce11900082ca.jpeg Hakimu aona hoja Sabaya, wenzake kujua hatma yao

Sat, 13 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imekiri washtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne wamekaa gerezani muda mrefu na wanastahili kujua hatma yao.

Aidha, imetaka upande wa jamhuri kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo Namba 2 ya Mwaka 2022 kwani ilistahili kuwa imeanza kusikilizwa. Kauli ya Hakimu Salome Mshasha inajibu hoja ya upande wa utetezi iliyowasilishwa na mawakili wa utetezi Moses Mahuna na Hellen Mahuna waliotaka mahakama kukamilisha upelelezi huo.

Hakimu alieleza kushangazwa kwake kwamba tangu kesi imepelekwa mahakamani hapo upande wa jamhuri umekuwa ukitoa sababu za kutokamilika kwa upelelezi, Sababu nyingine ni pamoja na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) kwamba hajatoa kibali kwa mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.

“Mahakama ipo kwa ajili ya kutoa haki na siyo kunyanyasa upande wowote, ni vyema upande wa jamhuri ukakamilisha upelelezi pamoja na kibali ili washtakiwa wajue haki zao,” alisema Hakimu Mshasha. Alisema mahakama haiwezi kuvumilia upande wa jamhuri kutoa sababu za aina moja kila wakati licha ya washtakiwa kuendeleza kuteseka bila kujua hatma yao.

“Nimesikiliza upande wa utetezi na nimebaini wana hoja, hatuwezi kuendeleza kuvumilia hili, huu ni muda wa kwenda msikitini, naahirisha shauri hadi Agosti 29, 2022 tutakapokuja kujibu vifungu vya sheria vinavyoainishwa na upande wa utetezi,” alisema. Akiwasilisha hoja, Wakili wa jamhuri Sabitina Mcharo aliiomba mahakama kuahirisha shauri kwa madai upelelezi haujakamilika pamoja na kutopatikana kwa kibali cha mahakama kuisikiliza kesi hiyo.

“Zipo hoja zinazotolewa na upande wa utetezi, tumezisikia na tutaziwasilisha kwa viongozi wetu kwa ajili ya utekelezaji,” alidai. Mapema akiwasilisha hoja za utetezi, Wakili Mahuna aliieleza mahakama kwamba sasa ni mwaka mmoja na miezi sita tangu washtakiwa kudaiwa kutenda kosa hilo.

“Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 22, 2021 hadi leo ni mwaka na miezi sita, na walifikishwa mahakamani Juni Mosi, mwaka 2022, tunaamini kwamba upelelezi ulitakiwa kuwa umekamilika lakini bado ni kinyume chake,” alidai Mahuna. Alisema wakati shauri hilo linafunguliwa walielezwa kwamba upelelezi umekamilika, lakini baadaye hoja zikabadilika na kudai haujakamilika, ni ombi la utetezi washtakiwa waachiwe hadi upelelezi ukamilike.

“Tangu kesi ifunguliwe Juni Mosi hadi leo ni miezi miwili imepitia nini kinasababisha upelelezi ukamilike, mahakama itazame Kifungu cha 62 Cha tafsiri ya sheria, kuwa endapo sheria haijatoka ukomo wa jambo kufanyika, jambo hilo linapaswa kufanyika kwa sababu za uzoefu,” alidai wakili huyo wa utetezi.

Alihoji kama upelelezi haujakamilika kwa nini washtakiwa hao walikamatwa na kuiomba mahakama imlazimishe DPP akamilishe upelelezi. Aliomba washtakiwa waachiwe na warejeshwe mahakamani mara upelelezi utakaokamilika ambapo mahakama iliahidi kujibu hoja hizo Agosti 29, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live