Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu amtaka Shamimu Mahakamani

Hakimu amtaka Shamimu Mahakamani

Thu, 16 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru mfanyabiashara, Shamimu Mwasha apelekwe katika mahakama hiyo ili aweze kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Shamimu ambaye ni mmiliki wa blog ya 8020 na mumewe Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida wanakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin kinyume cha sheria.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Aprili 15, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu, Jeneth Mtega kwa kuwa Shamimu hakufikishwa mahakamani hapo kutoka gereza la Segerea.

 

 

 

Pia Soma

Advertisement
Kutofika kwake kuliufanya upande wa mashtaka kuomba mahakama kutoa hati ya kumleta mshtakiwa huyo mahakamani hapo.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon amedai  kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo baada ya upelelezi kukamilika.

“Shauri lilikuja kwa ajili ya kuwasomewa maelezo mashahidi na vielelezo washtakiwa hawa, lakini hapa mahakamani yupo mshtakiwa mmoja (Nsembo) kutoka gereza la Keko na mshtakiwa wa pili yupo gereza na Segerea kama anavyoonekana kwa njia ya video.”

 

“Kutokana na hali hii hatuwezi kuwasomea maelezo yao, hivyo tunaiomba mahakama itoe hati ya kumleta mshtakiwa wa pili mahakamani hapa siku kesi hii itakapoitwa ili tuweze kuwasomea maelezo yao na kesi hii kuihamishia Mahakama Kuu,” amedai  wakili Simon.

 

Hakimu Mtega baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka aliamuru tarehe ijayo washtakiwa hao wapelekwe mahakamani ili waweze kusomewa maelezo yao.

 

Kesi hiyo imeahirishwa hadi April 29, 2020 itakapotajwa.

 

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa Kisutu  Mei 13, 2019 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019.

Wanandoa hao wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 232.70 wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Wanadaiwa kufanya kitendo hicho Mei Mosi, 2019 katika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Nsembo na Shamimu wanatetewa na wakili, Hajra Mungula na Charles Kisoka.

Chanzo: mwananchi.co.tz