Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu akerwa upelelezi kesi ya Zumaridi kuchelewa

Zumareed Pic Data Hakimu akerwa upelelezi kesi ya Zumaridi kuchelewa

Thu, 1 Sep 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Kesi namba 11/2022 inayomkabili Diana Bundala maarufu kama Mfalme Zumaridi peke yake imegeuka kuwa kaa la moto kwa Serikali baada ya mawakili wa utetezi kuhoji kwa nini upelelezi wa kesi hiyo haukamiliki wakati ni miezi sita tangu mteja wao ashikiliwe.

Hayo yamejitokeza jana Agosti 31, 2022 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Mwanza kwa hakimu anayesikiliza, Monica Ndyekobora huku mwendesha mashtaka wa serikali, Dorcas Akyoo akiieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Maelezo ya Akyoo yamepingwa vikali na jopo la mawakili wa utetezi likiongozwa na Wakili, Steven Kitale, Erick Mutta na Linus Amri ambapo wakili Kitale amesema suala la upelelezi wa kesi kutokamilika linachelewesha mteja wao kupata haki.

Kitale pia, amelitaka Jeshi la Polisi kuanza utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia aliyoyatoa hivi karibuni alipokuwa akifungua mafunzo kwa maofisa wa jeshi hilo mkoani Kilimanjaro ambapo alimtaka Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Ramadhani Kingai kukamilisha upelelezi kwanza ndiyo mtuhumiwa akamatwe.

 "Mheshimiwa hakimu naomba upande wa mashtaka wazingatie maelekezo ya mama yetu Rais Samia aliyotoa jana kwa Polisi. Ikiwezekana kesi ya Zumaridi iwe ya mfano kwa kumuachia ili wakafanye upelelezi wao wakatapokamilisha na ikabainika ana kosa ndiyo wamkamate," ameeleza Kitale

Katika hatua nyingine, Kitale ameieleza mahakama hiyo kuwa Mei 24 mwaka huu alimuandikia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) barua yenye kumbukumbu namba ONL/MWZ/VOL 02/54/2022 akilalamikia ucheleweshwaji wa shauri hilo linalomkabili mteja wake kwa kile kinachotajwa kuwa ni kutokamilika kwa upelelezi.

Kitale ameeleza kuwa katika aya ya pili ya barua hiyo alieleza wazi kwamba katika uendeshwaji wa kesi tajwa kumekuwepo na mahairisho mengi yasiyo na ukomo wala sababu zozote za msingi zaidi ya upande wa mashtaka kusema kuwa upelelezi haujakamilika.

Pia, ameieleza mahakama hiyo kuwa Jana Agosti 30, 2022 jopo la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo walimuandikia Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, John Kahyoza barua yenye kumbukumbu namba MAA/BR/CC.11/2022 likilalamikia shauri hilo kuahirishwa kwa zaidi ya miezi sita.

Katika maelezo yake, Kitale ameieleza mahakama hiyo kuwa sababu kubwa inayotajwa kusababisha shauri hilo kuahirishwa kuwa ni upelelezi wake kutokamilika na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka kisheria ya kusikiliza wala kutoa uamuzi juu ya mashtaka yanayomkabili mteja wao.

Kwenye barua hiyo pia, jopo la mawakili wa utetezi lilimuomba Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo kutumia mamlaka yake ya usimamizi kuliitisha jalada la kesi hiyo ili kulitolea maelekezo muhimu ikizingatiwa kwamba haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa.

Kwa upande wake, Hakimu Monica amemgeukia mwendesha mashtaka wa serikali, Dorcas Akyoo akimuuliza iwapo amesikia malalamiko yaliyowasilishwa na mawakili wa utetezi kuhusiana upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika huku Akyoo akikiri kupokea malalamiko hayo bila kueleza hatua zilizochukuliwa na upande wa Jamhuri.

Baada ya majibu ya Akyoo, Hakimu Monica ameeleza mahakamani hapo kuwa anakwenda kusoma sheria mbalimbali na kanuni ili kuona iwapo kuna kifungu kinachomruhusu kupeleka faili hilo katika ngazi ya juu.

"Suala hili liliwahi kulalamikiwa na mshtakiwa mwenyewe hapa mahamakamani, nikakuagiza mwendesha mashtaka ukamilishe upelelezi haraka iwekezanavyo lakini haujanipatia taarifa yoyote," ameeleza hakimu Monica

Ameongeza; "Sasa naenda kupitia sheria kama kuna kifungu kinaniruhusu kulipeleka ngazi ya juu nitafanya hivyo ili Septemba 9 mwaka huu tutakapokutana hapa nitoe maamuzi,"

Chanzo: www.mwananchi.co.tz