Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu akataa mdhamini wa Lissu kujitoa

48498 Pic+lissu

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa Robert Katula ambaye ni mdhamini wa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kujitoa baada ya kuieleza mahakama anaomba kujitoa kutokana na kukosa ushirikiano. 

Mbali na Lissu washtakiwa wengine ni Mhariri wa Gazeti la Mawio Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi.

Katula amedai leo Jumatatu Machi 25, 2019 Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba kuwa mshtakiwa wa nne hana taarifa naye na kwamba amekosa ushirikiano.

"Naomba kujitoa kutokana na kwamba sina taarifa ya mshtakiwa wa nne na nimejaribu kufuatilia lakini nimekosa ushirikiano," amedai Katula.

Wakili wa Serikali, Patrick Mwita amedai kuwa maneno aliyosema mdhamini kuwa mshtakiwa hajui alipo na jukumu lake ni kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani si sahihi hivyo kuomba kumpeleka mshtakiwa.

Mdhamini wa pili Ibrahim Ahmed alidai kuwa wametafuta kila namna ya kupata mawasiliano ya Lissu anakotibiwa hawakufanikiwa kumpata lakini kwa kuwa jukumu lake ni kufika mahakamani ameona ni vyema kufika na kutoa taarifa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba alieleza kuwa wamekuwa wakitegemea kupata maendeleo kutoka kwa wadhamini kwa ajili ya kuweka rekodi hivyo hakuna mdhamini atakayeweza kujitoa mshtakiwa akiwa hayupo mahakamani.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 25, 2019 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote wako nje kwa dhamana.

Washtakiwa hao kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Lissu yuko nje ya nchi tangu Septemba 7, 2018 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma. Mpaka sasa yuko nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu.



Chanzo: mwananchi.co.tz