Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu ahoji upelelezi mauaji ya mwanaharakati Wayne Lotter

48984 Mwanaharakatipic

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa kupambana na mauaji ya tembo, Wayne Lotter kupeleka taarifa sahihi ya jalada lilipo na hatua ya upelelezi ilipofikia.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Kalvin Mhina ameeleza leo Machi 27, 2019 baada ya Wakili wa Serikali, Jenifa Masue kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na jalada halisi bado liko kwenye hatua ya uchapwaji.

"Tarehe itakayopangwa mlete taarifa sahihi mahakamani, jalada liko wapi na kama upelelezi umekamilika," alisema Hakimu Mhina.

Mshtakiwa Robert Mwaipyana  alidai kuwa Machi 5, 2019

walitembelewa na mpelelezi wakiwa gerezani na kuelezwa kuwa upelelezi umeshakamilika na jalada liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka DPP.

Wakili Masue alidai kuwa Machi 25 alizungumza na mkuu wa upelelezi wilaya ya Kinondoni na kumweleza kuwa jalada liko hatua ya mwisho ya uchapwaji.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji namba 9 ya mwaka 2017 ni raia wa Burundi Habonimana Nyandwi na Nduimana Jonas maarufu Mchungaji (40) mkazi wa Kamenge, Burundi.

Wengine ni Godfrey Salamba (42) mkazi wa Kinondoni Msisiri A. Innocent Kimaro (23) mkazi wa Temeke Mikoroshini, Chambie Ally (32) mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa NBC, Robert Mwaipyana (31) mkazi wa Temeke Mikoroshini.

Wengine ni ofisa wa Benki ya Barclays, Khalid Mwinyi (33) mkazi wa Mikocheni B, Rahma Almas (37) mkazi wa Mbagala B na Mohammed Maganga (61) mchimba makaburi, Allan Mafue, Ismail Mohammed, Leornad Makoye, Amino Sham, Ayoub Selemani, Joseph Lukoa, Gaudence Matemu na Abuu Mkingie.

Katika kesi ya msingi washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Julai Mosi na Agosti 16, 2017 walikula njama ya kufanya mauaji ya Lotter.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa Agosti 16, 2017 katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selassie iliyopo wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, wanadaiwa kumuua Lotter.

Hakimu Mhina, aliahirisha kesi hiyo hadi  Aprili 10, mwaka huu itakapotajwa, washtakiwa wote wamerudishwa rumande kutokana na kesi ya mauaji inayowakabili kutokuwa na dhamana.

Uchapaji wa jalada kesi ya Wayne Lotter wakwamisha kesi kuendelea



Chanzo: mwananchi.co.tz