Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu ahoji mashahidi kutopelekwa mahakamani kesi ya Halima Mdee

78319 Mdee+pic

Thu, 3 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba ameutaka upande wa mashtaka kuwaleta mahakamani shahidi  wa kesi inayomkabili mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.

Amesema kutoletwa kwa shahidi kunampa wakati mgumu kuandika ripoti zake za kesi hiyo ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Ametoa kauli hiyo baada ya wakili wa Serikali, Wankyo Simon kuieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini shahidi waliokuwa wakimtegemea anaumwa na ameaga kuwa anakwenda  Hospitali.

"Shahidi alikuja hapa mahakamani kwa kujikongoja hivyo ameniaga ameenda hospitali, naiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine," amedai Simon.

Katika maelezo yake hakimu Simba amesema ameahirisha shauri hilo kwa muda mrefu na inamsumbua katika ripoti zake, kuutaka upande wa mashtaka kuhakikisha shauri hilo litakapotajwa tena mahakamani wawe na shahidi.

"Hakikisheni upande wa mashtaka  shauri hili linaendelea sio lazima awe shahidi mmoja mwingine akiumwa aje mwingine,” amesema hakimu Simba.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Wakili wa utetezi,  Peter Kibatala amedai upande wa mashtaka unadai shahidi anaumwa bila kutoa vielelezo vinavyoonyesha kama kweli  anaumwa.

Kibatala amedai anachofahamu ni kuwa shahidi huyo haumwi alikuwepo mahakamani hapo na walipomuuliza aliwaeleza anaenda kutoa ushahidi sehemu nyingine.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba ameahirisha shauri hilo hadi Oktoba 29 na 30, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kusikiliza ushahidi.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Halima alitamka maneno dhidi ya Rais Magufuli kuwa, “anaongea hovyo, anatakiwa afungwe breki,” kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz