Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu achachamaa, ataka mashahidi zaidi kesi ‘mhasibu’ Takukuru

29286 Pic+gugai TanzaniaWeb

Thu, 29 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kuhakikisha unapeleka mashahidi wa kutosha katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato chake  inayomkabili aliyekuwa  mhasibu mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai.

Gugai na wenzake watatu wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo,  19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali ambalo linamkabili Gugai pekee.

Uamuzi wa kuwaleta mashahidi wengi mahakamani hapo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kukosa  shahidi.

"Upande wa mashtaka nataka kesi hii itakapokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi mhakikishe mnaleta mashahidi wakutosha ikiwezekana mlete mashahidi hata watatu ili mmoja akipata udhuru,  mwingine aendelee na ushahidi ,” alisema Hakimu Simba.

 

“Nataka kesi hii ikamilike kwa wakati  maana ni ya muda mrefu. Naagiza upande wa mashtaka mhakikishe mnaleta mashahidi wa kutosha ikiwezekana baadhi ya kesi tutazisogeza mbele ili tuendelee na ushahidi wa kesi hii.”

 

Baada ya kueleza hayo aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 11 na 12 mwaka huu siku ambayo upande wa mashtaka utaendelea  na ushahidi.

 

Awali,  upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa shahidi aliyetakiwa kutoa ushahidi amehamishiwa Dodoma.

 

Tayari mashahidi wanne wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya Gugai.

 

Miongoni mwa mashahidi hayo ni Msajili wa Hati Msaidizi, kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Joanitha Kazinja.

 

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine, ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

 

Washtakiwa hao wanatetewa na jopo la mawakili,  Alex Mgongolwa,  Semi Malimi, Denis Tumaini, Nduluma Majembe na John Mhozya.

 

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake analodaiwa kutenda kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

 

Inadaiwa kuwa akiwa Takukuru Dar es Salaam, Gugai alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni ambazo hazilingani na kipato chake huku akishindwa kuzitolea maelezo.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz