Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakimu aahirisha kesi, ataka wafuasi wa Chadema wasiofika mahakamani wasakwe

53691 PIC+CHADEMA

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuwasomea maelezo ya awali (PH) washtakiwa 31 wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema kutokana na washtakiwa wengine 18 kutofika mahakamani. Washitakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya mkusanyiko usio halali.

Wakili wa Serikali, Faraji Nguka alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Agustin Rwizile kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusoma maelezo ya awali (PH) lakini kuna washtakiwa ambao waliomba hati za kuwakamata na bado wanaendelea kuwatafuta.

"Tupo tayari kuendelea na hoja za awali licha ya wafuasi 18 kutokuwepo mahakamani, tulishaomba hati za kuwakamata bado tunaendelea kuwatafuta," amedai Faraji Nguka.

Wakili wa kujitegemea, Majura Magafu amedai kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, huwezi kuendelea kama mshtakiwa hayupo mahakamani bila taarifa yoyote ya maandishi.

"Kesi inaruhusiwa kuendelea bila kuwakilishwa kama mshtakiwa atakuwa amewasiliana na wakili wake na kumpa taarifa tena kwa njia ya maandishi" amedai Wakili Magafu.

Wakili wa Utetezi, Alex Massaba amedai licha ya mahakama kutoa hati za kuwakamata washtakiwa, kumekuwa hakuna jitihada zozote za kuwatafuta.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Rwizile ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 17,mwaka huu kwa ajili ya kutolea uamuzi kama kesi hiyo iendelee na hoja za awali.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 51 ya  mwaka 2018,  ni Thabita Mkude, Haji Lukwambe, Emmanuel Kimoi, Mohammed Juma, Hussein Mrombo, Abdallah Hamis, Hussein Kidda, Paulo Kimoro, Brayan Morris, Hussein Nguli na Edna Kimoro.

Wengine ni Jonathan Lema, Salha Ngondo, Ramadhan Mombo, Godwin Mwakasungura, Hassan Kibweda, Omary Hamad, Fatima Ramadhan, Ezekiel Nyenyembe, Denis Mtegwa, Dickson Kerefu, Raphael Mwaipopo, Athuman Mkawa na Mussa Kusigila. Wengine ni Omary Danga, Jackson Masilingi, Asha Kileta, Ally Rajabu, Isack Ng'aga, Erick John na Aida Olomi.

Kwa pamoja wanadaiwa kuwa Februari 16, 2018 huko Kinondoni katika eneo la Mkwajuni, wilaya ya Kinondoni walifanya mkusanyiko usio wa halali na kinyume cha sheria. Ilidaiwa kuwa mkusanyiko huo ulikuwa na nia ya kufanya uvunjifu wa amani na kusababisha taharuki kwa wananchi.



Chanzo: mwananchi.co.tz