Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita: Polisi wapiga 'Stop' bodaboda kubeba wanafunzi

Digege Swalehe Digega akitangaza marufuku hiyo kwa madereva zaidi ya 200

Thu, 24 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la polisi mkoani Geita limepiga marufuku waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda kubeba wanafunzi wenye umri chini ya miaka tisa na wale wanaobeba watoto wengi kwa wakati mmoja kwa kuwa kitendo hicho ni ukatili na nikinyume na sheria ya usalama barabarani.

Akizungumza kwenye mafunzo  juu ya usalama, ulinzi kwa mtoto na ukatili wa kijinsia yaliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Plan International kwa bodaboda zaidi ya 200 wa mjini Geita, Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani hapa Swalehe Digega amesema kuanzia sasa dereva atakaekutwa amebeba watotoi wadogo atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Hii ni sheria nataka muitekeleze wewe beba wanafunzi  na wapo wanaobeba hadi watano kwa wakati mmoja hatutakukimbiza usijewaangusha ukasema  polisi wamesababisha tunachofanya ni kukupiga picha tutakufuata kijiweni kwako na kukukamata wakati wowote”amesema Digega

Aidha amewataka wazazi kutumia usafiri wa bajaji ambao ni rafiki kwa mtoto na kuwataka kutomkabidhi dereva mwanafunzi na badala yake kuongozana nao hadi shuleni kwa usalama zaidi wa mwanafunzi.

“Mnapowabeba kwa pikipiki mnawaweka mbele mnasababisha  madhara kwenye mapafu,wazazi zipo bajaji lakini huko hakikisha kuna mtu mzima anaongozana nao msiwaache wenyewe usalama wa mtoto unaanza na mzazi mwenyewe”alisema Digega.

Akizungumza na waendesha bodaboda waliopatiwa mafunzo hayo mkuu wa mkoa wa Geita Rosemary Senyamule aliwataka kuondoa ukatili wa kijinsia na wa watoto kwenye jamii kwa kutoa taarifa mapema pindi wanapoona matukio hayo.

Advertisement “Nyie mko kila maeneo elimu mliyoipata leo mkiamua kuitumia kwa kutoa ujumbe na mkiamua kutoa taarifa mnapoona ukatili mahali tutakua tumepunguza matukio haya kuanzia sasa badala ya kuwarubuni wanafunzi nyie ndio mgeuke kuwa walinzi wao”amesema Senyamule

Senyamule amesema yapo matendo yaliyokuwa yakifanywa na waendesha bodaboda bila kujua kuwa wanakwenda kinyume na haki za watoto na kwamba kupitia mafunzo hayo wamepata uelewa wa sheria,ulinzi na usalama wa mtoto.

Awali meneja wa Plan international mkoani hapa Adolf Kaindoa alisema kwa kutambua umuhimu wa kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na kwa kutambua umuhimu wa bodaboda katika kuwalinda watoto shirika hilo limetoa  elimu ya usalama na ulinzi wa mtoto kwa bodaboda zaidi ya 200 ili nao waweze kusambaza elimu hiyo kwa wengine.

“Jukumu la vijana wa bodaboda la kuwa watetezi wa watoto haliepukiki walioshiriki watapata mafunzo ya ukatili dhidi ya watoto,aina za ukatili,jinsi ya kutambua mtoto aliyefanyiwa ukatili,mtoto  aliyenyanyaswa,kutengwa nk”alisema Kaindoa.

Amesema kupitia mafunzo hayo wametengeneza jeshi jipya la wapambanaji wa kuzuia ukatili dhidi ya watoto na kwamba wanategemea kuona matokeo chanya kwa kuwa waliopatiwa mafunzo watafanya kazi kwa ukaribu na ofisi za kata ,idara ya ustawi wa jamii na jeshi la polisi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live