Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fuso lakamatwa likisafirisha sampuli za madini

43620 Pic+fuso Fuso lakamatwa likisafirisha sampuli za madini

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Mwanza inalishikilia gari lori aina Fuso lililokuwa likisafirisha shehena ya sampuli za madini kutoka mkoani Geita kwenda jijini humo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella jana alisema gari hilo lilikamatwa jana na ndoo 226 zenye sampuli za miamba ya madini 883 mali ya Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM).

“Gari hilo lilikamatwa na askari waliokuwa doria baada ya kubaini wahusika walikuwa na upungufu wa vibali vinavyoruhusu kusafirisha mzigo huo kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine,” alisema.

Mongella alisema shehena hiyo ilikuwa ikisafirishwa kwenda kwenye maabara ya kupima madini hayo ya SGS iliyopo jijini Mwanza.

Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa mkoa aliagiza kuchunguzwa na kufuatilia uhalali wa sampuli hizo huku akiwataka watendaji wa Serikali kufanya kazi kwa uadilifu.

Januari 4, mwaka huu walikamatwa watu sita wakiwa na kilo 323.6 za dhahabu na fedha taslimu Sh305 milioni zikisafirishwa kutoka Mwanza kwenda mkoani Geita.

Shehena hiyo ilikuwa kwenye gari aina ya Toyota Kruger likiwa na begi lililokuwa na mabulungutu ya fedha hizo ambapo watu 12 tayari wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Mwanza na kufunguliwa mashtaka kuhusiana na tuki hilo.

Washtakiwa hao wakiwamo askari polisi wanane wanaokabiliwa na shauri hilo ni aliyekuwa mkuu wa operesheni mkoa wa Mwanza, mrakibu mwandamizi wa polisi, Morice Okinda, E. 6948 D/CPL. Kasala, F. 1331 PL. Matete, G. 6885 D/C Alex na G. 5080 D/C Maingu.

Wengine ni G. 7244 D/C Timothy, G. 1876 D/C Japhet, H. 4060 D/C David Kadama, Hassan Saddiq, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda ambaye pia anafahamika kwa jina la Paulo Nkinda na Sajid Hassan.

Kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Januari 11, 2019 na kusomewa makosa saba yanayohusiana na uhujumu uchumi, rushwa na kutakatisha fedha.



Chanzo: mwananchi.co.tz