Katika hali isiyo ya kawaida, mkazi wa Mkuyuni jijini Mwanza, Juma Omary amejikuta akiangua kilio ndani ya chumba cha mahakama baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela muda mfupi baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kulawiti mtoto wa miaka mitano.
Hukumu ya Omary imetolewa leo Jumatatu Agosti 22, 2022 katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza na Hakimu mkazi wa mahakama ya Wilaya hiyo, Sheila Manento.
Katika kesi hiyo ya Jinai namba 87/2021, Omary ambaye ni fundi ujenzi mkoani Mwanza anadaiwa kumlawiti mtoto huyo ambaye ni wa jirani yake baada ya kumlaghai kumpatia kitu kitamu.
Hakimu Manento ameieleza mahakama hiyo kwamba ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wa upande wa mshtaka katika shauri hilo.
Hata hivyo, alivyopewa nafasi ya kujitetea, Omary ameieleza mahakama hiyo kwamba alikuwa amelewa ndiyo maana akatenda kosa hilo huku akiiomba mahakama hiyo imsamehe na kumwachia huru.
"Baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi wote wanne waliofika mahakamani hapa mahakama imejiridhisha na imekutia hatiani kwa kosa la kulawiti mtoto huyo. Hivyo mahakama hii inakuhukumu kifungo cha maisha jela," alisema Hakimu Manento.
Advertisement Hata baada ya hukumu hiyo kutolewa na alipochukuliwa na maofisa wa Polisi kwa ajili ya kupelekwa katika gereza la Butimba, mshtakiwa Juma Omary ameonekana akibubujikwa machozi.
Katika shauri lingine, mahakama hiyo imemhukumu mkazi wa Mabatini jijini Mwanza, Ismail Bulashi (49) kifungo cha maisha jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye miaka 10.
Hukumu hiyo imetolewa leo Agosti 22, 2022 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Veronica Mgendi.
Akisoma hukumu hiyo, Mgendi ameieleza mahakama hiyo kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo mwezi Machi 2022 baada ya kumdanganya mtoto huyo kwamba atampatia kitu pipi.
"Mahakama imejiridhisha na imekutia hatiani kwa kosa la kulawiti mtoto huyo. Hivyo inakuhukumu kifungo cha maisha jela," amesema Hakimu Mgendi
Awali, Wakili wa Mashtaka, Fortunata Guvette ameieleza mahakama hiyo kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo mwaka 2019 kinyume na kifungu namba 154 (1) na (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura namba 16 ya mwaka 2019.
Wakili huyo ameieleza mahakama kwamba mshtakiwa (Bulashi) alimdanganya mtoto huyo kwamba atampatia kitu kitamu kisha kumpeleka kichakani na kumfanyia ukatili huo.