Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fundi seremala asimulia alivyomuokoa mtoto aliyeibwa kanisani Dar

Video Archive
Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Saa 48 za kuibwa na kupatikana kwa mtoto Beauty Yohana (3) zimeendelea kuibua maswali mengi, safari hii aliyefanikisha mtoto huyo kupatikana ametoa simulizi yake.

Beauty, ambaye aliibiwa Jumapili iliyopita katika Kanisa la FPCT Mbezi Mwisho, jijini Dar es Salaam alipatikana juzi maeneo ya Kivule akiwa na msichana Angel Vicent (19) aliyedai kuwa mtoto huyo ni wa shangazi yake.

Alawi Muhammad ni kijana aliyewezesha kupatikana kwa mtoto huyo baada ya kupata taarifa za kupotea kwake katika kundi la mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Muhammad alikutana na Angel akiwa na Beauty kwenye mgahawa mmoja uliopo Kivule.

Akizungumza na Mwananchi jana, Muhammad alisema usiku wa Jumatatu iliyopita saa 2 usiku alikwenda kula chakula katika mgahawa huo na kumkuta mtoto huyo naye akila lakini akiwa peke yake, huku Angel akiwa ametoka nje.

Alisema baada ya kumwona mtoto huyo, aliikumbuka sura yake lakini hakujua aliwahi kumwona wapi.

Alisema baadaye alikumbuka kuwa alimuona mtoto Beauty kwenye kundi la WhatsApp akitangazwa kwamba amepotea.

“Nikiwa hapo nilitoa simu yangu kufananisha sura, nikagundua kwamba alikuwa mwenyewe. Nikamuuliza mhudumu, “huyu mtoto yuko na nani?”

Alisema mhudumu huyo alimjibu kuwa alikuwa na dada mmoja, lakini kwa muda huo alikuwa ametoka.

Muhammad, ambaye ni fundi seremala alisema baada ya muda mfupi, msichana huyo (Angel) akawa amefika.

“Huyo mtoto ni wa nani? Mbona anatafutwa? alihoji Muhammad akimlenga Angel, lakini msichana huyo alimjibu kuwa Beauty ni mtoto wa shangazi yake.

Alisema msichana huyo alisema binti huyo hawezi kutafutwa kwa kuwa yupo naye.

Muhammad alisema baada ya kujibiwa hivyo alishindwa kuendelea kumuuliza Angel na kudhani kwamba wakati mwingine mitandao ya kijamii huwa inapotosha.

Aliendelea kula na alipomaliza aliondoka na kuwaacha Angel na mtoto Beauty mgahawani hapo.

“Nilipofika nyumbani swali likanijia kichwani . Kama yuko kwa shangazi yake kwanini wale chakula mgahawani?” alijihoji Muhammad.

“Nililazimika kuingia tena katika mtandao wa WhatsApp na kuangalia namba nikapiga akapokea mwanamke ambaye alisema ndiyo mama wa mtoto,” alisema.

Alisema alimuuliza maswali mama huyo ili kujiridhisha kama kweli mtoto ni wake na amepotea.

Alisema baada ya kujiridhisha akamwambia kwamba amemuona mtoto huyo akiwa na msichana mmoja wakila chakula mgahawani.Kijana huyo alisema akiwa nyumbani usiku huo aliamua kurudi kwenye mgahawa, lakini alikuta wameshaondoka.

Muhammad alisema aliacha namba zake za simu kwa watu mbalimbali wanaofanya kazi kwenye eneo hilo akidai ni mtoto wa kaka yake ili akifika wampigie naye aje kumkamata.

Siku iliyofuata

Siku iliyofuata juzi Jumanne, Muhammad alisema alikwenda kibaruani na wakati akifungua mlango alipigiwa simu na mwanamke mmoja kwamba yule msichana (Angel) yuko pale mgahawani anakunywa chai.

“Nilimwambia mwanamke huyo wamzuie huyo dada asiondoke. Basi nilindoka faster (haraka) mpaka kwenye mgahawa huo, nikakuta tayari watu wameanza kujaa, nikawaambia wasimpige. Muda huo nikampigia simu mama yake akawa hapokei, kumbe alikuwa kwenye maombi,” alisema.

Mama alipotoka kwenye maombi akaikuta simu yake ina ujumbe kutoka kwa Muhammed ikimwambia apokee simu kwa sababu binti yake amepatikana.

Mama huyo anayeitwa Lucy Maganga alimwambia Muhammed asimkabidhi mtoto huyo kwa mtu yeyote kwa sababu alikuwa njiani kwenda kumchukua.

Muhammed alimtaka mama huyo wakutane polisi Kitunda kwa sababu polisi walikuwa wamefika kuwachukua.

Wazazi wa mtoto huyo walipofika kituo cha polisi cha Kitunda, Muhammad aliondoka na wao wakabaki kutoa maelezo kabla ya baadaye kupelekwa kituo cha polisi Stakishari ambako walitoa maelezo mengine na kutakiwa kwenda kituo cha polisi Gogoni ambako walifungua kesi.

Wazazi hao wakiambatana na askari mmoja waliondoka Stakishari kuelekea Gogoni na kutoa maelezo kwa saa mbili na kupewa PF3 kwa ajili ya uchunguzi wa mtoto.

Baba wa mtoto huyo, Yohana Isango alisema mwanaye alikaguliwa na askari wa kike ili kujiridhisha kama hajafanyiwa vitendo vibaya.

Alisema askari huyo hakubaini chochote na waliruhusiwa kurejea nyumbani na msichana huyo (Angel) kubaki kituoni hapo.

Mmiliki wa mgahawa

Mwanamke mwenye mgahawa huo, Rehema Hussein alisema msichana huyo alikwenda kula chakula Jumatatu usiku na Jumanne asubuhi akiwa na mtoto, lakini uhusiano wake na mtoto haukuwa mzuri na ulimpa mashaka.

“Alikuja hapa akaulizia bei ya chakula, nikamwambia, akaagiza wali, nikampelekea. Alikuwa akila peke yake, mtoto yeye hali. Kilipobaki kidogo ndiyo akampatia mtoto, naye akala kidogo akakiacha, muda wote mtoto alikuwa mnyonge,” alisimulia Rehema.

Rehema alisema kuna wakati mtoto alitaka kwenda kujisaidia nje lakini msichana huyo akamwambia kwa ukali “nenda kakojoe nje huko”. Alisema msaidizi wake alimchukua mtoto huyo na kumpeleka nje kujisaidia.

Alisema alipofika Muhammad na kuwaeleza kwamba huyo mtoto anatafutwa, alichukua namba yake na siku iliyofuata (Jumanne) asubuhi msichana huyo alipofika alimpigia simu ili aje kumkamata kama alivyokuwa ameomba.

“Yule dada ni katili sana, amejaa chale mwili mzima na anaongea kwa kujiamini sana. Asubuhi alikuja hapa kunywa chai bila kumpa mtoto, na kwa kuwa niliona hakula vizuri usiku uliopita ikabidi nimpatie chakula wakati msichana huyo amekamatwa,” alisema.

Wazazi saa 48 bila binti yao

Saa 48 za kutoweka kwa Beauty zilikuwa na maumivu makali kwa wazazi wake na kwa muda huo hawakulala wakihangaika kumtafuta kila kona ya Jiji la Dar es Salaam hasa katika maeneo ambayo waliambiwa kwamba msichana anayedaiwa kumwiba alionekana.

Baba wa mtoto huyo, Yohana Isango alisema alipata taarifa za kupotea kwa mtoto akiwa safarini kutoka Ngara na wakati huo alikuwa amefika Kibaha.

Alisema alimpigia simu mke wake akapokea simu huku akilia na kumwambia mtoto ameibwa.

Alisema baada ya kupokea simu hiyo alianza kuendesha lori kwa kasi ili awahi kufika nyumbani kufahamu kwa undani nini kimetokea.

Alisema alisimamishwa na trafiki mmoja akamwambia afukuzie gari kama anaweza, lakini alipofika kwenye mizani akakamatwa na trafiki wa pili, alipomweleza matatizo yake wakamruhusu aondoke.

“Kwa kawaida magari makubwa huwa tunaendesha kwa spidi 70 lakini nilianza kuendesha kwa spidi 100 na zaidi. Maeneno mengi nilikuwa nina-overtake bila kujua na nilikamatwa na trafiki kwa kosa la kupita kwenye zebra, siyo mwendo kasi,” alisema.

Kuku wachinjwa

Alisema kwa kawaida huwa anatoka na kuku mikoani kwa ajili ya familia yake na siku hiyo alikuwa na kuku wanne lakini kutokana na tukio la kupotea kwa mwanaye, hawakupata mlaji lakini jana ndiyo wamewachinja kufurahia.

Isango alisema watu wengi walikuwa wanakwenda nyumbani kwake kumfariji na walikuwa wanapokea simu nyingi kutoka kwa watu wa mikoa mbalimbali wakimpa pole na kumwombea mtoto wake apatikane.

“Watanzania wametuonyesha ushirikiano mkubwa, tulipotoa taarifa tu kwenye mitandao ya kijamii watu wakaanza kutupigia simu. Ninawashukuru pia Mwananchi kwa kuandika habari hii, mmetupa ushirikiano mkubwa mpaka leo (jana),” alisema Isango.

Alisisitiza kwamba kupatikana kwa mtoto huyo kumetokana na nguvu kubwa ya maombi ya Watanzania ambao wakati wote walikuwa pamoja naye. Aliwashukuru pia waumini wa kanisa la FPCT Mbezi kwa kusaidia kumtafuta mtoto wake.

Tukio lahusishwa na ushirikina

Mama wa mtoto huyo, Lucy Maganga alidai kuwa msichana aliyemuiba mtoto wake alikuwa na ushirikina, lakini ameshindwa kutokana na maombi ambayo wamekuwa wakifanya tangu kupotea kwake.

Alisema msichana huyo alikiri kwamba alimwiba mtoto huyo kwa ajili ya kumpeleka kwa bibi mmoja ambaye huwa anawatuma kwa ajili ya kuwatoa kafara. Alisema binti huyo aliwaambia kwamba alipompeleka Beauty, bibi huyo alimwambia anataka mtoto wa kiume.

“Ninaweza kusema huyu msichana alikuwa na nguvu za giza kwa sababu kila alipokwenda watu walikuwa wakimuona lakini wanakosa ujasiri wa kumkamata, akiondoka tu ndiyo wanakumbuka kumkamata. Hata ukimwangalia mwilini amejaa chale mwili mzima,” alisema.

Lucy alisema tangu mwanaye ameibiwa alikosa usingizi na muda mwingi alikuwa akiomba Mungu apatikane. Alisema alipokea simu kutoka kwa watu mbalimbali na wengine walifika nyumbani kwake na kufanya maombi pamoja.

“Siku ambayo mtoto aliibiwa niliishiwa nguvu na nilikuwa nikitetemeka. Kilichoniumiza ni kutojua mtoto yuko wapi, ana hali gani, anakula nini na amelala wapi. Nilikuwa na maumivu ya nyonga kwa sababu ya ujauzito wangu lakini nguvu zilikuja ghafla, nikaanza kutembea kumtafuta huku na huko,” alisema.

Maganga alisema baada ya kutofanikiwa kumpata, alikwenda kanisani wakafanya maombi kisha akaongozana na shemasi wa kanisa hilo pamoja na baadhi ya vijana wa kanisa hilo kwenda kuripoti polisi katika kituo cha Gogoni.

Taarifa za kupatikana mtoto

Alisema juzi alfajiri alikuwa kwenye maombi kama kawaida na alipotoka kwenye majira ya saa 3 asubuhi alikuta simu 25 zilizopigwa bila kupokelewa na ujumbe kutoka kwa Muhammad ukisema “pokea simu, mtoto kapatikana.”

Alisema muda huohuo, akampigia Muhammad na kumwambia asimkabidhi mtoto kwa mtu yoyote mpaka atakapofika kwani wakati huo alianza safari kutoka Mbezi na kuelekea Kivule na kufanikiwa kuwakuta katika kituo cha polisi cha Kitunda.

“Tunamshukuru sana huyu kaka pamoja na Watanzania wote ambao walikuwa pamoja nasi kwenye maombi mpaka kuwezesha kupatikana kwa mtoto huyu, haikuwa kazi rahisi lakini kwa nguvu ya maombi imewezekana,” alisema mama huyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz