Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fundi nguo aliyetekwa na watu wasiojulikana apatikana

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Fundi wa nguo na muuza vitambaa vya suti katika soko la Mugumu wilayani Serengeti, Juma Siki (34) aliyehofiwa kutekwa na watu wasiojulikana ambao waliomba kupewa Sh15milioni ili wamuachie, amepatikana akiwa hai.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki, fundi nguo huyo amepatikana jana usiku Jumatatu Mei 27, 2019.

Akizungumza na Mwananchi leo, Ndaki  amesema Siki aliyetekwa Jumamosi iliyopita Mei 25, 2019 amepatikana  wilayani Bunda.

“Amepatikana jana usiku alifika polisi Bunda kwa Bodaboda akapelekwa hospitali kwa matibabu, sasa hivi tunaendelea na mahojiano atueleze mkasa mzima," amesema Ndaki.

Kamanda huyo ameagiza kijana huyo kupelekwa Mugumu Serengeti lilipotokea tukio hilo kwa ajili ya mahojiano.

Taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu wa Siki zinaeleza kuwa hakuwa katika hali mbaya ya kiafya siku aliyopatikana.

Pia Soma

“Alitueleza kuwa alipigwa na ubapa wa panga kisha akafungwa kitambaa usoni. Amesema alijikuta sehemu ambayo haitambui na aliomba msaada wa Bodaboda hadi polisi," amesema mmoja wa ndugu zake.

Baada ya kutekwa kwa Saki Kamanda Ndaki alisema wanafuatilia kubaini wahusika kupitia simu ya Juma ambayo imetumika kutuma ujumbe kwa rafiki yake ukimtaka atumiwe Sh15 milioni ndipo wamuachie huku ukieleza kuwa bado yupo hai.

Alieleza kuwa  ndani ya gari ya Juma aina ya Toyota Noah lililokutwa karibu na nyumba yake walikuta damu, kisu, mawe na vitu vingine ambavyo inadaiwa vilitumiwa na watuhumiwa wa tukio hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu alilieleza tukio hilo akidai limewastua na askari wanaendelea na ufuatiliaji na ameomba watu wenye taarifa sahihi wasaidie ili watuhumiwa waweze kukamatwa.

Sirikwa Marwa aliyedai ni rafiki mkubwa wa  Juma alikiri kupokea ujumbe wa simu kupitia namba ya rafiki yake ukimtaka ajitahidi kutuma kiasi hicho cha fedha.

Chanzo: mwananchi.co.tz