Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fundi ETDCO mbaroni akituhumiwa kuiba nyaya za transfoma 13

90208 Nnnpic Fundi ETDCO mbaroni akituhumiwa kuiba nyaya za transfoma 13

Mon, 30 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Handeni. Jeshi la polisi mkoani Tanga nchini Tanzania, linamshikilia Masia Naumbe (30) mfanyakazi wa kampuni tanzu ya Tanesco ya ETDCO inayofanya kazi ya kujenga na kubadilisha miundombinu ya umeme chakavu kwa  tuhuma ya kukutwa na nyaya aina ya shaba ambazo ameiba kwenye transfoma mbalimbali zenye thamani ya Sh156 milioni.

Leo Jumamosi, Desemba 28, 2019 Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe amekiri jeshi hilo kumshikilia mfanyakazi huyo wa kampuni ya ETDCO kwa kukutwa na nyara hizo za Serikali ambazo ni mali ya Tanesco alizozipata kwa njia ya wizi.

Amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu kwani ameshakiri kuhusika na kufanya kitendo hicho.

"Mtuhumiwa hakulisumbua jeshi la polisi kwani amekiri kuhusika na kuiba nyaya hizo, hivyo siku ya Jumatatu tunamfikisha mahakamani kusomewa kesi yake ya kukutwa na nyaya hizo," amesema Bukombe.

Mejena wa Tanesco wilaya ya Handeni, Meshack Masanyiwa amesema jumla ya transfoma 13 nyaya zake za shaba zimeibwa ambazo kati ya hizo 10 ni mali ya Tanesco na tatu mali ya kampuni ya ETDCO ambao ndio mtumishi wao amehusika katika suala hilo.

"Kukatwa kwa nyaya hizo madhara yake ni transfoma kuungua na kuleta hitilafu za umeme kwa wananchi, hivyo Tanesco imepata hasara ya Sh12 milioni kwa kila transfoma na kwa transfoma zote 13 ni sawa na hasara ya Sh156 milioni," amesema Masanyiwa.

Uchunguzi wa kubaini wizi wa nyaya hizo ulifanywa katika transfoma 20 na 13 kubainika ndio nyaya zake zimeibwa hivyo zilizobakia salama ni transfoma saba tu.

Chanzo: mwananchi.co.tz