Kuishi kwingi, kuona mengi! Ndivyo anavyosema Philipo Matakope (64), mkazi wa Kitongoji cha Mimbi Kata ya Kitongosima, wilayani Magu mkoani Mwanza, ambaye hajui hatima ya usalama wa miguu yake, hasa wa kulia anaohofia umevunjika kutokana na alichodai ni kipigo kutoka kwa walinzi wa mwekezaji aliye jirani na eneo lake.
Matakope, baba wa watoto 10 waliozaliwa na mkewe Maza Kisimba (50), anadaiwa kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili na walinzi hao usiku wa kuamkia Agosti 19, baada ya kukutwa ndani ya mipaka ya eneo la jirani yake alikoingia akifukuzana na fisi aliowakurupusha zizini kwake.
Licha ya kushindwa kunyanyuka ikidaiwa ni kutokana na kipigo hicho kilichosababisha miguu yote miwili kushindwa kufanya kazi, Matakope aliyelazwa kwa matibabu katika wodi ya wanaume Hospitali ya Wilaya ya Magu, hazungumzi chochote zaidi ya kububujikwa machozi pindi ndugu, jamaa na marafiki wanapomsemesha.
Mwanahabari alimshuhudia mzee huyo aliyelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu akiwa amefungwa plasta ngumu kwenye mguu wake wa kulia huku mguu wa kushoto, kifua na mgongo pia kukiwa na majeraha.
Simulizi ya familia
Akielezea tukio hilo, mke wa mzee Matakope alisema usiku wa kuamkia Agosti 19, kundi la fisi lilivamia nyumbani kwao ndipo mumewe aliamka kwenda kukabiliana nao wasidhuru mifugo yao.
“Kabla ya siku hiyo, mbuzi wetu watano waliliwa na fisi na siku waliporejea tena mume wangu aliamua kutoka nje ili akawafukuze wasije kutumalizia mifugo, ningejua haya yangetokea ningemzuia asitoke maana maisha yake ni muhimu kwetu kuliko mifugo. Lakini ndio hivyo tena binadamu hatujui yajayo,” alisema Kisimba.
Aliongeza “Akiwa huko nje, nilisikia vishindo na kelele za mume wangu kukimbizana na fisi hao na baadaye hali ikatulia. Sikuwa na hofu kwa sababu nilijua baada ya kuwafukuza, lazima baba atakuwa amejificha sehemu kuvizia hadi ahakikishe fisi hawarudi tena. Lakini ajabu ni kwamba hakurejea hadi nilipopitiwa usingizi.”
Alisema asubuhi ya Agosti 20, Mwenyekiti wa Kitongoji hicho , Msoga Blandashi alifika nyumbani kwake kumtaarifu kuwa mumewe amekamatwa na yuko chini ya ulinzi kwa jirani yao mwekezaji kutoka China na hali yake siyo nzuri, hawezi kunyanyuka wala kutembea.
Alisema walinzi hao wamekuwa wakiwakamata mtu yeyote anayekutwa au kukatiza kwenye eneo la mwekezaji huyo ambalo halina uzio wala alama.
Inadiwa walinzi wake huwakamata watu hata wakiwa nje ya eneo lao kwa sababu wanalipwa bonasi ya Sh50, 000 kila wanapomfikisha mtu kwa Mchina.
“Uongozi wa Jeshi la Polisi na Serikali ya mtaa uliingilia kati suala la mume wangu na kufanikiwa kumchukua kutoka mikononi mwa walinzi wa Mchina na kumpeleka hospitali kwa matibabu. Tunamwomba Mungu apone aje asimulie kilichomtokea,” alisema mama huyo
Kiini cha uhasama
Akizungumza na Mwananchi juzi, James Philipo (26), mmoja wa watoto wa mzee Matakope, alisema familia yake imekuwa na mvutano na mwekezaji huyo kwa kuwa waligomea fidia iliyotolewa ili wahame kama walivyofanya baadhi ya wakazi ili kumpisha mwekezaji.
“Utamaduni wetu Wasukuma huwezi kuhama na kuacha makaburi ya ndugu zako ndiyo maana baba alikataa mpaka fidia hiyo itakapohusisha gharama za kuhamisha makaburi ya ndugu zake.”
Aliziomba mamlaka husika kuingilia kati suala hilo alilosema limeifanya familia yao kuishi kwa hofu, hasa baada ya majirani wengine kukubali kupokea fidia na kuhama wakiachwa pekee yao eneo hilo.
“Familia yangu haina uwezo wa kupambana na watu wenye fedha, tunaiomba Serikali kupitia vyombo vyake ichunguze tukio la kujeruhiwa kwa baba yangu na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria hata kama aliingia eneo la mwekezaji hawakustahili kumpiga, wangemfikisha polisi na kumshtaki,” alisema James
Kauli ya mwekezaji
Akizungumza na Mwananchi kupitia kwa mkalimani wake, Meneja wa Kiwanda cha Tanfresh kinachotekeleza mradi wa ufugaji wa samaki kata ya Kitongosima, Chengdeng Chen, alikiri mzee Matakope kukamatwa na walinzi wake usiku wa kuamkia Agosti 19 na baadaye kukabidhiwa kwa askari wa Jeshi la Polisi kituo cha Nyaguge.
Kuhusu mgogoro kati ya kiwanda na familia ya mzee Matakope, meneja huyo alisema; “Mimi sina mamlaka ya kujadili fidia na mkazi wa eneo hili kwa sababu nina mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambao hujadiliana na wananchi ni kiasi gani cha fidia walipwe kupisha mradi.”
Meneja huyo aliwatupia lawama wakazi wa eneo hilo kuwa wanahujumu mradi wa kufuga samaki kwenye vizimba kwa kufanya vitendo vya kihalifu ikiwamo wizi wa mali mbalimbali kama mifuniko vya vizimba na hivyo kusababisha hasara kwa vifaranga vya samaki kukimbilia ziwani.
DC, DED Magu
Akizungumza na Mwananchi kuhusu uhasama kati ya mwekezaji na tukio la mzee Matakope kudaiwa kupigwa na walinzi wa mwekezaji, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kali alisema ofisi yake inafuatilia suala hilo kwa karibu kujua kilichotokea huku akiahidi kulizungumzia baada ya kupokea taarifa za kiuchunguzi kutoka kwa vyombo vya dola.
“Kwa sasa ninachoshauri ni ninyi waandishi kufika hospitali mzungumze na Mganga Mfawidhi kujua hali ya mgonjwa,” alisema DC Kali aliyewahi kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza.
Juhudi za kupata taarifa za hali ya mgonjwa kama alivyoelekeza Mkuu huyo wa Wilaya hazikufanikiwa baada ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Magu, Dk Masele Luhende kugoma kuzungumza hadi apate kibali cha maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.
Majerugi ana nakala ya Fomu Namba Tatu (PF3) yenye kesi namba NYG/RB/786/2022 iliyojazwa Agosti 19, na askari namba G.8297 Koplo Mwita wa Kituo cha Polisi Nyaguge Wilaya ya Magu inayoonyesha kuwa mzee huyo alipata majeraha yaliyosababishwa na kipigo.