Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia yapigwa na butwaa kusikia aliyempa mimba mtoto wao amejiua

26484 Pic+mimba TanzaniaWeb

Sun, 11 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Familia ya Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kisangura wilayani hapa, wamesema kujiua kwa askari Magereza, Yohana Tangawizi muda mfupi baada ya kutajwa kumpa mimba mtoto wao, kumewachanganya.

Tangawizi aliyekuwa na cheo cha sajenti katika Gereza la Mradi Tabora B, alijiua kwa kujipiga risasi mbili mdomoni nyumbani kwake Novemba 9 na kabla ya kujiua, aliacha ujumbe wa maandishi ukisema alijiua kwa sbabu ya kuumwa tumbo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki juzi aliliambia Mwananchi kuwa Tangawizi alikuwa amefunguliwa jalada katika kituo cha polisi akituhumiwa kumpa mimba mwanafunzi wa sekondari.

Jana, Shukurani Joseph (47) ambaye ni baba mzazi wa mwanafunzi huyo, akizungumza na Mwananchi kwa simu alisema alitegemea mtuhumiwa angefikishwa katika vyombo vya sheria kwa kitendo hicho, lakini sasa hajui atafanya nini.

“Kwa sasa kama familia, hatujui tufanye nini maana aliyetajwa na mwanangu kuwa alimpa mimba inaonekana alipewa taarifa na polisi na kuchukua uamuzi huo mgumu, ingawa ujumbe alioacha ni tofauti na tukio, hili limetuchanganya,” alisema Joseph.

Joseph ambaye ni kiongozi wa kikundi cha Kwiyengo cha Kanisa la Wasabato Bonchugu, Kata ya Sedeko alisema hakuwa na taarifa kama mwanaye ana ujauzito wa miezi minne hadi alipoitwa na kuelezwa na mkuu wa shule Novemba 5.

“Nilipofika niliambiwa kuhusu suala hilo sikuamini, niliamua kumchukua mwenyewe na kumpeleka Zahanati ya Bonchugu, akapimwa na tarehe sita nikafuata majibu ndipo ikabainika kuwa ni mjamzito, mbele ya mwalimu alimtaja aliyempa mimba na kutoa namba ya simu waliyokuwa wakiwasiliana naye,” alisema.

Alisema Novemba 7, alipewa barua na mkuu wa shule kupitia kwa Mtendaji wa Kata ya Kisangura ili ampeleke binti yake Kituo cha Polisi Mugumu kutoa taarifa na polisi walitaka apelekwe tena hospitali kupimwa ili wajiridhishe kama ni mjamzito.

“Mtoto wangu na mwingine wa sekondari ya Nyamoko walipelekwa kwenye vipimo na polisi na kubainika wa kwangu ana mimba ya miezi minne na yule mwingine miezi mitano, wakawekwa ndani wote kama washtakiwa wakisubiri waliowapa mimba wakamatwe,” alisema.

Hata hivyo, alisema alipofuatilia Polisi Novemba 8, aliulizwa kama ameenda kumchukua mtoto wake. “Nilishangazwa na swali hilo, mimi nilitegemea kumkuta mtuhumiwa waliyesema watamtafuta wamkamate, lakini wakawa wananiuliza eti kama namhitaji mwanangu nimchukue, nikawaambia nahitaji kujua kinachoendelea.”

Joseph alisema aliitwa na mkuu wa upelelezi wa wilaya na kuomba wazungumze, ndipo akamweleza kilichotokea kwa mtuhumiwa muda mfupi baada ya kufungua jalada hilo. “Nilimuuliza nani alimpa taarifa, akasema hata yeye hajui, niliumia.”

Kuhusu hatima ya mwanaye Joseph alisema hajui kwa kuwa wanategemea kuanza mitihani ya kidato cha pili Jumatatu kama ataruhusiwa, lakini wakimkatalia kama familia kwa sasa hatujui cha kufanya.



Chanzo: mwananchi.co.tz