Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia ya Sheikh Gora aliyotoweka miezi minane iliyopita yaililia polisi

65849 Pic+gora

Mon, 8 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Ni miezi minane sasa tangu Mkuu wa chuo cha Dini cha Thanawi cha Nyakato Islamic Institute kilichopo chini ya Taasisi ya The Registered Trustee of Islamic ya jijini hapa, Sheikh Bashiri Gora atoweke katika mazingira yenye utata.

Kutokana na hali hiyo, wanafamilia wa sheikh huyo wameipigia magoti wakiomba isaidie kumsaka kwani haijui iwapo yu hai au la.

Akizungumza na Mwananchi jana, Safina Said ambaye ni Sheikh Gora alisema tangu Desemba 6 mwaka jana, maisha yao yamebadilika kuanzia kuishi kwa hofu hadi uchumi kudorora. Alisema Sheikh Gora alikuwa mwalimu hivyo maisha yao hayakuwa ya kubahatisha kama ilivyo kwa sasa.

“Tangu niolewe sikuwahi kusikia kwamba mume wangu ana matatizo au ugomvi na mtu yeyote. Nashindwa kuelewa kiini cha yeye kutekwa na kupelekwa kusikojulikana. Mume wangu alikuwa kila kitu hapa nyumbani. Kwa sasa maisha ninayoyapitia ni magumu na changamoto lukuki,” alisema Safina.

Alisema kabla mumewe hajatekwa, alikuwa akifanya biashara ndogondogo, lakini amelazimika kutumia mtaji wake kuwalisha watoto na sasa hana fedha.

“Kwa sasa naishi kwa msaada, nyumbani kwetu wananisaidia na pia kwa mume wangu wanatoa mkono wa huruma kwa wanangu hawa.”

Pia Soma

Alisema majuma kadhaa yaliyopita walifuatilia suala hilo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro ambaye aliwajibu kuwa bado wanachunguza.

Hata jana alipoulizwa na Mwananchi kuhusu hilo alijibu kuwa bado polisi wanaendelea na upelelezi.

Farida Rashid, ambaye ni mke mdogo wa Sheikh Gora, mwenye watoto wawili pia alisema kwa sasa maisha yao yamebadilika na kila siku anamuombea mumewe arudi nyumbani akiwa salama.

“Alikuwa kila kitu, mimi sina kazi yoyote ninayoifanya kwa hiyo napitia wakati mgumu sana kuwalisha wanangu,” alisema Farida.

Mussa Ali Gora, mdogo wa Sheikh Gora ambaye pia ni mwalimu chuoni hapo alisema hana uhakika kama kweli kaka yake atapatikana akiwa hai kwa kuwa suala la kumtafuta limechukua muda mrefu.

“Ni vigumu kubashiri kwa kweli ingawa polisi wanasema jitihada za upelelezi zinaendelea,” alisema.

Alivyotoweka

Katibu wa Bodi ya Taasisi ya The Registered Trustee of Islamic, Sadik Mchola alisema siku ya tukio, wakiwa chuoni hapo alifika kijana mmoja kuulizia nafasi ya kujiunga na chuo hicho kwa ajili ya mdogo wake.

“Kijana huyo alitukuta ofisini, Sheikh akamwambia aje Januari (2019) atapewa utaratibu, kijana aliondoka lakini baada ya muda kidogo akarudi tena kuulizia malipo, Sheikh akamwambia Januari ndiyo tutakueleza kila kitu, akaondoka.

“Baada ya saa moja na nusu kupita, akarudi tena akasema baba amesema unipe namba ya simu. Sheikh akamwandikia akampa lakini mimi nikamuuliza unatokea wapi na unakaa wapi? Akajibu anatoka mtaa wa chini hapo Temeke, baba yangu amepanga hapo kuna jumba la ghorofa ila baba yangu anakaa Dar, huku amekuja kikazi.”

Kwa mujibu wa maelezo ya Mchola, kijana huyo aliwaeleza kuwa yupo kidato cha tatu sekondari moja ambayo ipo Bunda, Mara. “Nikamwabia wewe unaonaje ukaja kusoma hapa kwenye shule yetu? Akasema sawa nitaongea na baba lakini baada ya saa moja na nusu akarudi tena na Sh10,000 kwa ajili ya kuchukua fomu ya kujiunga na shule, akapelekwa kwa mkuu wa shule.”

“Baada ya hapo, wakawa wanazungumza na Sheikh huku anamsindikiza kumbe walikuwa wameegesha gari nyuma ya chuo, walipokaribia, alitoka kijana mwingine kwenye gari hiyo wakambeba Sheikh na kumuingiza ndani kisha gari likaondoka kwa spidi kali.”

Taasisi hiyo iliyopo Nyakato wilayani Nyamagana, inamiliki shule ya awali, msingi na sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

Akizungumzia matukio ya utekaji, mwanaharakati Habibu Mchange alisema kupoteapotea na kutekwa kwa watu kusihusishwe na siasa pekee, bali matukio hayo yachunguzwe kwa jicho la tatu.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakizua tafaruku na kwenda mafichoni na baadaye kusemekana kwamba wametekwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz