Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia sheikh aliyetekwa yahofia watoto kukosa ada

35031 Pic+familia Familia ya Sheikh Bashir Gora

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Wakati shule nyingi zikifunguliwa kesho, familia ya Sheikh Bashir Gora, mkuu wa Chuo cha Kiislamu Nyakato jijini hapa, anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana mwezi uliopita, imeingiwa na hofu ya watoto kushindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa ada.

Sheikh Gora alichukuliwa kwa nguvu na kuingizwa kwenye gari na watu wasiojulikana Desemba 6, 2018 alipokuwa eneo la ofisi zake ambapo hadi jana alikuwa hajapatikana.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, mke mdogo wa Sheikh Gora, Farida Rashid alisema licha ya simanzi na hofu kwa wanafamilia, kutoweka kwa sheikh huyo kumeiacha familia bila mlezi na kipato cha uhakika.

“Kutoweka kwake kunaiumiza sana familia hasa kipindi hiki shule zinapofunguliwa, watoto wanahitaji ada na gharama zingine ambazo hatuwezi kuzimudu, hatujui tutafanyaje. Lakini inaweza kufikia hatua watoto wakashindwa kwenda shule, hatukujipanga, hatujui pa kuanzia,” alisema.

“Mwanzoni jambo hili lilionekana kama utani eti mtu anatekwa na watu na kutokomea naye mchana kweupe, lakini kadri siku zinavyoyoyoma bila kupatikana tunazidi kupata wakati mgumu kwa sababu ndiye aliyekuwa kila kitu na nguzo ya familia.”

Januari Mosi, familia ya Sheikh Gora mwenye wake wawili na watoto saba ilifanya dua maalumu iliyofanyika nyumbani kwake eneo la Nyamhongolo katika Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya kumuomba Mungu asaidie kupatikana kwake.

Ingawa dua hiyo ilifanyika kwa faragha, mdogo wa sheikh huyo, Khalili Gora aliliambia Mwananchi kuwa maombi hayo pia yalilenga kuviongezea nguvu na ujuzi vyombo vya dola katika juhudi za kumtafuta na kumpata akiwa hai.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vinaendelea kumtafuta sheikh huyo, huku akitoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake kuzitoa polisi au kwa viongozi wa Serikali wa maeneo yao.



Chanzo: mwananchi.co.tz