Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Faini ya Sh500 milioni ilivyowatoa jela washtakiwa wa dhahabu

49623 FAINI+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Januari 9, Rais John Magufuli alizungumzia namna ‘mchongo’ wa utoroshaji madini ulivyofanyika mkoani Mwanza, akiwatuhumu askari wasiokuwa waaminifu kuwa nyuma ya mpango huo.

Rais alizungumzia sakata hilo wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua akiwemo Waziri wa Madini, Doto Biteko.

Alitumia nafasi hiyo kumpongeza mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kufanikisha kukamatwa watuhumiwa na polisi hao.

Baada ya kukamatwa watuhumiwa walifikishwa mahakamani.

Ilivyokuwa

Kati ya Januari 4 na 5, watu 12 walikamatwa wakisafirisha kilo 319.59 za dhahabu na fedha taslimu Sh305 milioni kwenda nchi jirani ya Rwanda.

Katika tukio hilo, wafanyabiashara wanne-Hassan Sadiq, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda na Sajid Hassan- ambao ndio wenye mali hizo pamoja na askari wanane walitiwa mbaroni Sengerema wakiwa na kiasi hicho cha dhahabu na fedha, kabla ya kufunguliwa mashtaka.

Wafanyabiashara hao sasa wapo huru baada ya kukiri makosa yao, mahakama kuwatia hatiani kwa makosa sita na kuamuru waende gerezani kutumikia kifungo cha kati ya miaka mitano hadi 15 au kulipa faini ya kati ya Sh5 milioni hadi Sh100 milioni. Kwa ujumla wao walilipa jumla ya Sh529.8 milioni na kukwepa kifungo.

Makosa waliyotiwa nayo hatiani ni pamoja na kutakatisha fedha, kujihusisha na vitendo vya rushwa na kukutwa na madini kinyume na sheria.

Mahakamani mara ya kwanza

Watu hao walifikishwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Januari 11 na kusomewa mashtaka saba yanayohusiana na uhujumu uchumi, rushwa na utakatishaji fedha mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Gway Sumaye.

Februari 11, upande wa utetezi ulilalamika mahakamani hapo kukosa fursa ya kuonana na kuzungumza na wateja wao hao wawapo gerezani na hata wanapofikishwa mahakamani.

Kwa nyakati tofauti mawakili wao, Anthony Nasimile na Nazalio Michael waliiomba mahakama kuwapa fursa hiyo. Akijibu maombi ya mawakili hao, Hakimu Sumaye alisema washtakiwa hao wana haki ya kuonana na mawakili ingawa si jukumu la kupanga huku akiwataka kufuata taratibu, ikibidi muda na siku za kuonana nao mahabusu.

Washindwa kufika mahakamani

Februari 25, washtakiwa hao hawakufikishwa mahakamani. Hata hivyo hakukuwa na taarifa iliyotolewa ya sababu ya kutofikishwa kwao. Siyo mawakili wa Serikali, wa utetezi wala Hakimu Sumaye waliokuwa na sababu ya kutofikishwa kwao, badala yake Hakimu alisema hakupata taarifa zozote kuhusu washtakiwa hao.

Na alipoulizwa wakili wa Serikali Castuce Ndamugaba, naye alidai kutofahamu sababu huku akiomba waulizwe polisi.

Hakimu aliahirisha shauri hilo na kupanga Machi 13, hata hivyo siku hiyo shauri hilo liliahirishwa kutokana na upelelezi kutokamilika.

Wakiri kosa na kutolewa hukumu

Machi 27, shauri hilo lilianza kusikilizwa saa nne asubuhi hadi saa 12:20 jioni chini ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Rhoda Ngimilanga.

Kabla ya kuanza kusikilizwa, mkurugenzi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Fredrick Manyanda aliiomba mahakama kubadilisha hati ya mashtaka na kuipa mamlaka mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo - ombi lililokubaliwa na mahakama. Hivyo, washtakiwa hao walisomewa hati mpya iliyokuwa na makosa 10 yakiwemo ya kutakatisha fedha, kuomba na kupokea rushwa na kujihusisha na rushwa. Baada ya wakili wa Serikali, Robert Kidando kuwasomea mashtaka wanne kati ya 12 walikiri makosa na wengine waliyakana.

Hukumu, fedha na dhahabu vyataifishwa

Baada ya kukiri makosa yao sita, Hakimu Ngimilanga aliwatia hatiani na kuwahukumu kulipa faini tofauti kati ya Sh5 milioni na Sh100 milioni au kifungo cha miaka kati ya mitano hadi 15. Mbali na adhabu hiyo pia mahakama iliamuru kutaifishwa dhahabu hiyo, magari mawili waliyokutwa nayo, mashine ya kupimia dhahabu na Sh305 milioni walizokutwa nazo.

Kutokana na muda kuwa ulikuwa umekwenda watu hao hawakuweza kulipa faini hiyo, hivyo walipelekwa rumande hadi siku iliyofuata, Machi 28 walipokamilisha taratibu za kulipa.

Hakimu Ngimilanga aliliambia Mwananchi kwamba kwa sasa wapo huru baada ya wote wanne kufanikiwa kulipa faini.

Wakati wenzao wakikiri makosa, kuhukumiwa, kulipa faini na kutoka gerezani, washtakiwa wanane ambao wote walikuwa askari akiwemo aliyekuwa mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mwanza, Morice Okinda walikana mashtaka na kesi yao itaendelea kusikilizwa Aprili 10 baada ya upelelezi kukamilika. Wengine ambao kesi dhidi yao inaendelea ni E. 6948 D/CPL. Kasala, F. 1331 PL. Matete, G. 6885 D/C Alex, G. 5080 D/C Maingu, G. 7244 D/C Timothy, G. 1876 D/C Japhet na H. 4060 D/C David Kadama.

Soma zaidi> Washtakiwa kesi ya dhahabu wakacha kifungo, walipa faini



Chanzo: mwananchi.co.tz