Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Faini au jela kwa kusafirisha na kumiliki dhahabu kinyume

5a13873a4f01654e176906af7fa6427e Faini au jela kwa kusafirisha na kumiliki dhahabu kinyume

Sun, 25 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu raia wa India, Piyushkumar Shah kulipa faini ya Sh milioni 10 au kwenda jela miaka miwili baada ya kutiwa hatiani makosa mawili ya kusafirisha na kumiliki madini ya dhahabu yenye thamani ya Sh milioni 2.5 kinyume na sheria sambamba na kutaifishwa madini hayo kuwa mali ya serikali.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaid.

Kabla ya kusoma hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Nguka Faraji alisoma maelezo ya mashtaka kwa mshtakiwa ambaye alikiri makosa yote.

Katika maelezo hayo Nguka alidai katika kosa la kwanza, Aprili 10, 2021 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam mshtakiwa huyo alikutwa akisafirisha kipande cha dhahabu chenye uzito wa gramu 20 cha thamani ya Sh 2,592,007.77 mali ya Serikali ya Tanzania kinyume na sheria.

Alidai pia katika shitaka lingine tarehe na mhali hapo hapo mshtakiwa huyo alikutwa akimiliki kiasi hicho cha madini mali ya serikali ya Tanzania kinyume na sheria.

Aidha, wakili Nguka aliwasilisha mahakamani hapo vielelezo sita ikiwemo hati ya ukamataji, Ripoti ya uthamini, tiketi ya elektroniki, lasi ya kusafiria, simu ya mkononi, kompyuta mpakato na madini hayo.

Baada ya kusoma maelezo hayo Wakili Nguka aliieleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo ni mkosaji kwa mara ya kwanza na hana kumbukumbu za uhalifu lakini aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Wakati wa shufaa upande wa utetezi uliiomba mahakama kutoa adhabu ya chini kwa kuzingatia kuwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza kama ilivyoelezwa na upande wa mashtaka lakini pia alionesha tabia njema kwa kukiri haraka na kuokoa muda wa mahakama pia kwa kuzingatia tahamani ya madini aliyokamatwa nayo mshtakiwa alionesha wazi kuwa hakuwa na nia ovu.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Hakimu Shaidi alisema hukumu yake ilijikita katika maelezo ya pande zote mbili.

“Kama ilivyosemwa na upande wa mashtaka kuwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza na huna kumbukumbu za jinai na pia umekiri mapema nimeamua kukupa adhabu ya kulipa faini iliyotamkwa kisheria hivyo utalipa faini ya milioni tano au kwenda jela miaka miwili kwa kosa la kwanza na adhabu hiyo hiyo kwa kosa la pili, rufaa iko wazi kwa yeyote ambaye hajaridhika na adhabu hii,” alimaliza kusema Hakimu Shaidi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz