Moja ya Masoko makubwa ya kihalifu duniani yanayotumiwa na walaghai wa mitandaoni kununua nenosiri (password) limefungwa baada ya operesheni kubwa iliyofanywa na maafisa usalama.
Soko hilo liitwalo Genesis Market lilikuwa likiuza maelezo ama taarifa za kuingilia kwenye akaunti za mitandaoni, anuani za IP zinazotumika kubaini vifaa au mtandao ndani ya intaneti, taarifa ambazo ziliweza kufoji alama za vidole kidigitali n.k.
Baadhi ya nenosiri zilizokuwa zikiuzwa sana kwenye soko hilo ni zile za kuingilia kwenye mitandao kama Facebook, PayPal, Netflix, Amazon, eBay na Airbnb. Wahalifu waliokuwa wakinunua taarifa hizo walikuwa wakipewa taarifa ikiwa nenosiri litabadilishwa.
Mashirika ya usalama kutoka nchi 17 duniani yalikuwa sehemu ya zoezi hili kubwa lililoongozwa na FBI wa Marekani wakishirikiana na Mamlaka ya Polisi ya Uholanzi, Shirika la kitaifa la uhalifu la nchini Uingereza NCA, Mamlaka ya polisi ya Australia na nchi zingine za Ulaya.
Katika zoezi la kuuangusha mtandao huo watu 120 wanaosadikiwa kuhusika na matumizi ya soko hilo walikamatwa kwa makosa ya ulaghai na matumizi mabaya ya kompyuta.