Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Elimu ya vita rushwa ya ngono shuleni isambazwe kote nchini

Rusha Ya Ngono Unyanyasajii wa kingono ni changamoto inayokabili jamii yetu

Wed, 30 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rushwa ya ngono imekua ikitajwa katika shule za msingi, sekondari na vyuo, ikichangia kukwamisha baadhi ya wanafunzi wa kike kutimiza ndoto zao katika elimu wanaponaswa na rushwa.

Tuhuma za rushwa ya ngono kwa wanafunzi, huwa zinawaangukia madereva wa bodaboda, bajaji, daladala, walimu na hata watu wazima mitaani wanaotumia mbinu mbalimbali kuhakikisha wanawanasa mabinti.

Mfano hai ni pale madereva wanapotumiwa kuwarubuni kwa lifti, ili kuwawahisha shuleni huku walimu wakitumia ahadi za kuwapa majibu ya mitihani, lakini kwa wengine mitaani wakidaiwa kutumia fedha zao kuwanasa.

Hata hivyo, kuna jitihada mbalimbali zinazofanywa na taasisi za serikali zikiwamo Taaisisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kushirikiana na wadau wanaopambana na vitendo hivyo, ili kuhakikisha vinakomeshwa.

Miongoni mwa jitahada hizo imo ya wiki iliyopita ya semina ya walimu walezi wa klabu za kupinga rushwa kwenye shule za msingi na sekondari jijini Dodoma, iliyoandaliwa na TAKUKURU.

Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka, katika halfa hiyo anawataka walimu walezi wa klabu za kupinga rushwa kuwajenga wanafunzi uadilifu na uzalendo wa mapambano dhidi ya rushwa wakiwa shuleni.

Anataka walimu wasaidie taasisi hiyo kufanikisha elimu ya kuzuia rushwa inawafikia wanafunzi kwa ufasaha, huku akiipongeza TAKUKURU kuanzisha klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi na sekondari mkoani humo.

Kimsingi, tatizo la rushwa ya ngono kwa wanafunzi limeenea nchi nzima, hivyo kwa mtazamo wangu ni kwamba kama mikoa mingine itaiga mfano ulioanzishwa na TAKUKURU Mkoa wa Dodoma.

Ninaamini kwamba, iwapo mfano huo utaigwa itakuwa ni rahisi shule zote nchini kuwa na klabu hizo za kupinga rushwa na ngono na kuwafanya wanafunzi kuwa na uelewa wa kutosha wa kupambana na rushwa hiyo.

Inawezekana wapo baadhi ya wanafunzi hawajui madhara ya ngono, wengine wanaweza kuwa wanajua lakini wanashindwa kujisimamia, hivyo kuwapo semina, klabu zao shuleni vinaweza kuwabadilisha wakawa makini.

TAKUKURU wakifika kila nchini na kutoa semina kuhusu madhara ya rushwa ya ngono, hatua hiyo inaweza kuongeza kasi ya uelewa kwa wanafunzi wanaosomea katika mazingira hatarishi.

Ikumbukwe kuwa wapo baadhi ya wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kwenda shule na kurudi nyingine, wengine wanaishi katika nyumba za kupanga mitaani kutokana na shule kutokuwa na mabweni.

Mazingira hayo ni hatarishi kwa mwanafunzi wa kike, kwani ndiyo ambayo huwaingiza kwenye vishawishi vya kupewa lifti ili wawahi shule au kurubuniwa kwa ahadi za kulipiwa kodi huko wanakopanga mitaani.

Kuwapo semina za kila mara zinazotolewa na TAKUKURU kwa kila shule nchini, kutasaidia kudhibiti rushwa ya ngono hata kugundulika na kupungua haraka, kwani wahusika watakuwa wameelewa madhara yake na jinsi ya kuikwepa.

Vivyo hivyo, nao TAKUKURU wakitoa semina kwa wanafunzi kila mara na kuwaelekeza wapi pa kushtaki wanapokutana na rushwa hizo, itawarahisishia kukataa unyonge wa lifti, kupewa majibu ya mitihani au fedha.

Nionavyo, si vibaya kuendelea kuongeza walimu wa kike wengi shuleni na kuwapandisha vyeo, ili

viwafanye angalau wawepo ni watu wawili wa juu wanaotoa uamuzi katika shule husika na kufuatilia kwa ufasaha mienendo ya wanafunzi wa kike, wakiwapa semina za malezi kuwaondoa katika hatari ya mahusiano.

Njia hizo zinaweza kusaidia kuwafanya wanafunzi ambao wapo katika klabu za kupambana na rushwa ya ngono kuwa mabalozi watakaosaidia kuwaimarisha wenzao katika vita hiyo inayohatarisha maendeleo yao kielimu.

Ni hatua inayotokana na ukweli kwamba, klabu hizo za shuleni zinawasaidia wanafunzi kubadilishana mawazo na kupeana uzoefu na mikakati ya kupambana na rushwa hiyo nyumbani, mitaani, njiani na shuleni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live