Jeshi la Polisi nchini Hispania wamekamata droni tatu zisizo na rubani za kutumiwa chini ya maji zilizotengenezwa kusafirisha dawa za kulevya katika bahari kutoka Morocco.
Droni hizo zina uwezo wa kubeba hadi kilo 200 za mizigo. Kama sehemu ya uchunguzi wa miezi 14, watu wanane wamekamatwa katika miji ya Cadiz, Malaga na Barcelona.
Polisi wanasema ina maana kwamba wamevunja genge linaloshukiwa kujenga magari hayo na kuyasambaza kwa walanguzi wa dawa za kulevya kote Ulaya.
Polisi wa Uhispania wanasema ni mara ya kwanza kugundua gari la chini ya maji lenye uwezo wa kuendeshwa bila mtu.
"Vifaa hivi vinaweza kuruhusu walanguzi wa dawa za kulevya kusafirisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kwa mbali katika Mlango-Bahari wa Gibraltar," polisi walisema katika taarifa.
Mlango-Bahari wa Gibraltar ni ukanda mwembamba wa bahari unaotenganisha Moroko na Uhispania.
Nyambizi moja ilijengwa kabisa na nyingine mbili zilikuwa bado zinaendelea kujengwa. Inaaminika mbili zilikuwa zikijengwa ili kusafirisha kokeini.
Maafisa pia walikamata kilo 14 za hashish, kilo 8 (lbs 18) za bangi, zaidi ya €157,300 (£135,527) pesa taslimu, na ndege sita kubwa zisizo na rubani.