Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Tenga, wenzake waomba siku 14 maombi yao kwa DPP kusikilizwa

77482 Pic+tenga

Sat, 28 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Byrson Shayo, wakili wa washtakiwa watano akiwemo, Dk Ringo Tenga ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwapa siku 14 ili maombi ya barua ya wateja wake kukiri makosa yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kujibiwa.

Wakili wa washtakiwa hao, Byrson Shayo ameieleza mahakama hiyo leo Ijumaa Septemba 27, 2019 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Dk Tenga ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni ya mawasiliano ya Six Telecoms Limited na wenzake, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 73/2019.

Washtakiwa hao  wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.

Wakili Shayo amedai  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa wamejadiliana na wateja wao na baada ya majadiliano hayo wameamua kumuandikia DPP barua kwa kuzingatia maagizo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa Septemba 22,  2019.

" Wateja wetu (washtakiwa) Septemba 26, 2019 walimuandikia DPP barua yenye maombi mbalimbali kuhusiana na shauri hili,” amedai Shayo.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement

Amesema kutokana na uamuzi huo, wanaiomba mahakama kutoa ahirisho la siku 14 kuanzia leo ili waweze kupata  majibu ya barua hiyo.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 11, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande

Awali, wakili wa Serikali, Jackline   Nyantori amedai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba Septemba 23, 2019 upande wa utetezi uliwasilisha ombi mahakamani hapo wakiomba kuja kujadiliana na wateja wao.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa hao ni  Alex Mgongolwa, Semi Malima, Constancia Sospeter, Jeremiah Mtobesya na Shayo.

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.

Katika kesi ya msingi, Dk Ringo na wenzake wanadaiwa kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14, 2016 Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa  chini ya kiwango cha Dola za Marekani  0.25 kwa  dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia, katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya TCRA kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao wanadaiwa  katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shitaka la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni, Tenga na Chacha, wanadaiwa walitumia ama walisimamia Dola za Marekani 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashtaka yaliyotangulia.

Vile vile ,washitakiwa hao wanadaiwa kuisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22.

Chanzo: mwananchi.co.tz