Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Pima, wenzake wakwama kuanza kujitetea

Pima Mkurugenzi Jiuji Dk Pima, wenzake wakwama kuanza kujitetea

Tue, 18 Apr 2023 Chanzo: mwanachidigital

Upande wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha,Dk John Pima na wenzake wawili,umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwapa muda wa siku moja kwa ajili ya kujibu notisi ya kuwasilisha nakala halisi ya nyaraka 14 zilizoombwa na upande wa utetezi.

jana jumatatu Aprili 17,2023, mahakama hiyo ilipanga kuendelea na shauri hilo la uhujumu uchumi namba 5/2022,kwa upande wa washitakiwa kuanza kujitetea ila ilishindikana kufuatia maombi hayo ya Jamhuri.

Mbele ya Hakimu Mkazi Serafini Nsana anayesikiliza kesi hiyo, Wakili wa Serikali mwandamizi, Hebel Kihaka aliiomba mahakama iwape muda wa siku moja kwa ajili ya kujibu notisi hiyo ambapo alidai kuwa iliwasilishwa mahakamani hapo Machi 20,2023 ila wao wamepewa nakala hiyo jana Aprili 17.

Wakili huyo aliiomba mahakama itoe ahirisho la siku moja (leo) kwa ajili ya kwenda kufuatilia nyaraka hizo kwenye vyombo vya uchunguzi.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022 inayosikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,mbali na Dk Pima watuhumiwa wengine ni aliyekuwa Mweka hazina wa Jiji hilo Mariam Mshana na aliyekuwa Mchumi, Innocent Maduhu.

Wakili Kihaka aliieleza mahakama kuwa notisi hiyo inaomba nyaraka 14 na imeambatanisha majina ya nyaraka hizo ambapo 12 kati ya hizo zinatoka kampuni ya Cherry General Supply and Services,mkataba wa mauzo ya gari baina ya Maduhu na Jackson Lugome ya Aprili 7,2022 na maelezo ya shahidi chini ya kifungu cha 10(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ua ya Juma Kihamia.

"Kati ya vyote vilivyoorodheshwa ni maelezo tu ya shahidi ndiyo ambayo tuna ufahamu nayo ila hizo nyaraka nyingine 13 tunahitaji uhakiki kwa kufanya mawasiliano na vyombo vya uchunguzi kwa maana katika shauri hili sisi kama Jamhuri hatuna na hatujawahi kuwa na nakala hizo halisi,"

"Notisi waliyowasilisha mahakamani inaeleza nyaraka hizo zinategemewa na washitakiwa wote watatu pamoja na kwamba hawatazitumia leo na hatujui ni wakati gani watazitumia,"alieleza

Akijibu kwa niaba ya utetezi, Wakili Mpaya Kamala,alieeleza kuwa wanakubaliana na maombi hayo ya kufanya mawasiliano na vyombo vya uchunguzi na kuomba waendelee na utetezi kwani hawatatumia nyaraka hizo.

"Kwa kuwa muda walioomba sio mrefu tunakubaliana nao lakini kwa leo tunaomba tuendelee na ushahidi wa utetezi kwani leo hatutatumia hata mojawapo ya nyaraka hizo,"alieleza Wakili Kamala

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Serafini alikubaliana na ombi la Jamhuri na kuahirisha shauri hilo hadi kesho Aprili 17 litakapoendelea.

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka tisa ikiwemo kosa la utakatishaji fedha Sh103 milioni.

Chanzo: mwanachidigital