Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Pima aeleza alivyomtuma dereva wake kuweka fedha benki

HUKUMU Dk Pima aeleza alivyomtuma dereva wake kuweka fedha benki

Fri, 21 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa muamala wa Sh10 milioni aliomtuma dereva wake akamuwekee kwenye akaunti yake binafsi Machi 29, 2022 siyo sehemu ya Sh103 milioni wanazoshitakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili na wenzake wawili.

jana Aprili 20, 2023, Dk Pima ameendelea kutoa utetezi wake ikiwa ni siku ya tatu mbele ya Hakimu Mkazi Serafini Nsana anayesikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022 ambapo washitakiwa wengine ni Mariam Mshana (aliyekuwa mwekahazina) na Innocent Maduhu aliyekuwa mchumi.

Akiongozwa na Wakili wake wa utetezi Mpaya Kamala, Dk Pima amedai mahakamani hapo kuwa hajawahi kupewa kiasi cha Sh10 milioni na Maduhu kati ya Machi 23 hadi Mei 25, 2022 kama wanavyoshitakiwa.

Amedai kuwa shahidi wa 19 wa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, Sara Jastine alidai Machi 29,2022 alimuona na kumhudumia (Dk Pima) katika benki ya NMB tawi la Mazengo ambapo aliweka katika akaunti yake Sh10 milioni.

Pia amedai shahidi wa 26 wa Jamhuri alidai taarifa fiche zilimwambia aliweka fedha hizo kwenye akaunti yake mwenyewe.

Ameendelea kudai kuwa kuanzia Machi 28 hadi 30, mwaka jana alikuwa Dodoma na washitakiwa wenzake wawili, maofisa wa bajeti kutoka jiji la Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Katibu Tawala mkoa wa Arusha kwa ajili ya vikao vya bajeti kufuatia mwaliko uliokuwa umetolewa na Katibu Mkuu Ofis ya Rais Tamisemi kwa Makatibu Tawala mikoa yote Tanzania Bara.

Alidai kuwa kikao cha Machi 28, 2022 kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala mkoa wa Arusha kila halmashauri iwakilishwa na mkurugenzi, mwekahazina na mkuu wa Idara ya Mipango, ufuatiliaji na maafisa bajeti.

Pia amesema Machi 29, kilifanyika kikao cha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, aliyewaalika Makatibu Tawala wa mikoa yaote nchini na wakurugenzi wa halmashauri zote nchini, wawekahazina na maafisa mipango kutoka halmashauri zote Tanzania Bara.

"Machi 29 hiyo hiyo Mkoa wa Arusha ulikaa tena na Tamisemi kupitia vitabu vya bajeti baada ya kikao cha Katibu Mkuu asubuhi na kilihusisha wakurugenzi wote halmashauri za Mkoa wa Arusha, waweka hazina na maafisa mipango.

“Machi 30, 2022 mkoa wa Arusha uliitwa mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya bajeti na utawala na kuwasilisha mpango na bajeti wa mkoa wa Arusha na halmashauri zake zote saba," amesema.

Hakimu Nsana ameahirisha kesi hiyo hadi kesho Aprili 21, 2023 itakapoendelea kusikilizwa kwa shahidi huyo kuendelea na utetezi wake.

Katika kesi hiyo washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa tisa ikiwemo utakatishaji fedha Sh103 milioni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live