Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diwani akatwa mapanga, aporwa Sh5 milioni taslimu

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kahama. Diwani wa Sabasabini katika Halmashauri ya Ushetu, Kahama mkoani Shinyanga, Emmanuel Makashi amenusurika kifo baada ya kushambuliwa kwa kukatwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi nyumbani kwake usiku wa kuamkia jana.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Richard Obwao alisema katika tukio hilo, wavamizi hao walimpora diwani huyo fedha taslimu Sh5 milioni.

“Ni vyema wananchi wakajenga tabia ya kuhifadhi fedha benki badala ya kukaa majumbani na kiasi kikubwa cha fedha na hivyo kuvutia wahalifu,” alisema.

“Katika purukushani za kupora fedha hizo, diwani Makashi alijeruhiwa kwa kukatwa mapanga alipojaribu kukabiliana na wavamizi hao ambao majina wala idadi yao haijajulikana,” alisema.

Alisema wakati wakitimka mbio baada ya kupora na kujeruhi, mmoja wa watuhumiwa aliyetambuliwa kwa jina la Yohana Masanja (19), mkazi wa Kijiji cha Lowa alikamatwa na kushambuliwa hadi kufa na wananchi waliojitokeza baada ya kusikia kelele za kuomba msaada.

Baada ya kumuua, wananchi hao walimteketeza kwa moto.

Akizungumza kwa simu akiwa katika Hospitali ya Mji wa Kahama alikopelekwa kwa matibabu, Makashi aliwashukuru wananchi waliojitokeza kumsaidia wakati wa tukio hilo kitendo ambacho alisema kiliwafanya watuhumiwa kutimua mbio.



Chanzo: mwananchi.co.tz