Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diwani Athumani atajwa kesi ya mauaji ya dada wa bilionea Msuya

Diwanii Diwani Athumani

Sun, 13 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

OFISA wa Polisi, Mrakibu (SP) Latifa Mohammed, amedai hafahamu kama aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Diwani Athumani, ndiye alitoa maelekezo mke wa marehemu Bilionea Msuya, Miriam Mrita, arekodiwe video.

Pia amedai kuwa hafahamu kama CP Diwani ni kaka wa marehemu Aneth Msuya na hafahamu kama alikuwa akiongoza migogoro ya ndugu.

SP Latifa alidai hayo jana Mahakama Kuu mbele ya Jaji Edwin Kakolaki wakati akitoa ushahidi kwenye kesi ya mauaji inayomkabili Miriam na mwenzake ambao wanadaiwa kumuua dada wa Bilionea Msuya, Aneth Msuya.

Akiongozwa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, alidai alikwenda Arusha Agosti 4, 2016 kwa ajili ya kumkamata Miriam kwa tuhuma za mauaji yaliyotokea maeneo ya Kibada, Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Alidai kuwa katika safari yake aliongozana na SP Jumanne Malangahe na Mrakibu Msaidizi (ASP) David Mhanaya lakini hafahamu kama Jumanne anajulikana nchi nzima kwa kutesa watuhumiwa.

Shahidi alidai kuwa alikuwa anafahamu jina la aliyekuwa anakwenda kumkamata na tuhuma za mauaji zinazomkabili. Pia alidai alimkamata maeneo ya Tembo Club lakini hakuwa na hati ya kumkamata, akidai kifungo namba 14 cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) kilimruhusu.

Wakili Kibatala alimpa sheria hiyo asome kifungu kilichomruhusu lakini shahidi alikaa kimya kwa dakika kadhaa bila majibu.

Kibala alisoma kifungu kimoja baada ya kingine lakini hakukuwa na kifungu wala mazingira yaliyoruhusu SP Latifa kumkamata mtuhumiwa bila hati ya ukamataji.

Shahidi alidai walikuwa na hati ya upekuzi, baada ya kumkamata walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake maeneo ya Sakina, Arusha.

Pia alidai kuwa katika upekuzi walichukua nguo aina ya suti jozi mbili, viatu jozi mbili na kadi za magari lakini hajui magari hayo yalihusikaje katika tukio la mauaji.

Shahidi alidai kuwa alimhoji mshtakiwa kwa mdomo huku ASP David akichukua video wakati wa mahojiano hayo lakini akadai kuwa katika kifungu namba 57 cha CPA, hakuna mahali palipoandikwa mahojiano yachukuliwe kwa kurekodi video isipokuwa kuna palipoandikwa mahojiano kwa njia ya mdomo.

Wakili Kibatala alihoji kama shahidi anafahamu kuwa maelekezo ya kumrekodi video mshtakiwa Miriam yalitoka kwa aliyekuwa DCI wakati huo, Kamishna Athumani.

Kibatala alihoji kama anafahamu kuwa Diwani ni kaka wa marehemu Aneth Msuya na akahoji kama anafahamu kuwa migogoro ya ndugu ilikuwa ikiongozwa na Athumani.

Shahidi alidai hafahamu kama David alipewa maelekezo na Kamishna Diwani Athumani kurekodi video na hafahamu kama ni kaka wa marehemu Aneth Msuya na hafahamu kama alikuwa akiongoza migogoro ya ndugu.

SP Latifa alidai walikamata gari aina ya Suzuki Vitara lenye namba za usajili T620 CBB, gari T677 BNM Toyota Landcruiser na T800 CKF Range Rover lakini hajui yalihusikaje katika tukio la mauaji.

Wakati akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Geses Tesha, shahidi alidai walikwenda kumkamata mtuhumiwa Agosti 4, 2016 Arusha na Agosti 5 walimkamata Tembo Club.

Alidai baada ya kumkamata walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake, walichukua nguo na viatu na baada ya kukamilisha upekuzi walirejea Dar es Salaam .

Latifa alidai walimfikishia Kituo cha Polisi Chang'ombe na Agosti 8, 2016 walifanya mahojiano naye kwa mdomo na kwa kumrekodi video.

Alidai kuwa Afande David alikuwa akirekodi video, mtuhumiwa alieleza mpango mzima wa mauaji, alionyesha maeneo waliyokuwa wanakutana kabla ya tukio na baada ya tukio la mauaji maeneo ya Kibada.

Katika kesi hiyo ya mauaji washtakiwa ni mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara, Revocatus Muyella.

Katika kesi ya msingi namba 103/2018, washtakiwa hao wanadaiwa kumuuwa kwa kukusudia Aneth Msuya, dada wa marehemu bilionea Msuya Mei 25, 2016 maeneo ya Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live