Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam nchini Tanzania imepanga Agosti 5, 2019 kusikiliza maombi ya dhamana ya Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi, Agosti Mosi,2019 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Augustine Rwizile, baada ya upande wa mashtaka kuomba Mahakama hiyo kuleta kiapo kinzani.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai mahakamani hapo kuwa upande wa mashtaka wamepokea maombi hayo leo Alhamisi hivyo wanaomba muda wa kuyapitia na kuwasilisha hati kinzani.
Uamuzi wa kusikiliza shauri hilo, Jumatatu ijayo, unatokana na Maombi ya dhamana namba 14/ 2019 yaliwasilishwa jana Mahakamani hapo na Wakili wa kutoka Mtandao wa Utetezi wa Haki za binadamu, Shilinde Swedy.
Katika maombi hayo, Swedy anaomba mteja wake ambaye ni Kabendera apatiwe dhamana au afikishwe mahakamani.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Rwezile aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 5, 2019, ambapo mahakama hiyo itasikiliza maombi ya dhamana ya upande wa utetezi.
Habari zinazohusiana na hii
- Uhamiaji Tanzania yachukua paspoti saba nyumbani kwa Kabendera
- Polisi Tanzania kuzungumzia sakata la mwandishi wa habari aliyechukuliwa kwa nguvu
- Mwandishi wa habari Tanzania achukuliwa kwa nguvu nyumbani kwake, polisi wakana
Baada ya kuchukuliwa, mwandishi huyo anayeandikia magazeti ya ndani na nje ya Tanzania amekuwa akihojiwa kuhusu uraia wake ambapo jana Jumatano, Idara ya Uhamiaji ilikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake, Mbweni na kufanikiwa kuchukua paspoti saba ambapo moja ni ya kwake zingine za ndugu zake.