Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dhamana washitakiwa saba kesi ya wafuasi wa Chadema shakani

8980 Cdm+pic TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

 Dar es Salaam.  Washtakiwa saba, kati ya 31 wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, wamenusurika kukamatwa na kufutiwa dhamana baada kushindwa kufika mahakamani kusikiliza shauri lao.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya mikusanyiko isiyo halali na kinyume cha sheria, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hatua hiyo imefikiwa leo Juni 12, baada ya Wakili wa Serikali Ester Martin, kuieleza Mahakama, mbele ya Hakimu Mkazi, Karim Mushi, kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini kuna baadhi ya washtakiwa katika kesi hiyo, hawajafika mahakamani hapo.

Wakili huyo, kabla ya kuendelea na shauri hilo, aliita majina ya washtakiwa, kuanzia mshtakiwa wa kwanza hadi wa 31na ndipo alipobaini washtakiwa saba kati ya 31, hawapo mahakamani hapo.

Ester aliwataja washtakiwa hao saba ambao hawakufika Mahakamani hapo  bila kutoa taarifa kuwa ni Edna Kimoro, Jonathan Lema, Ramadhan Mombo, Ezekiel Nyenyembe, Raphael Mwaipopo, Athuman Mkawa na Jackson Masilingi.

 “Mheshimwa hakimu, washtakiwa saba kati 31 wanaokabiliwa na shtaka la kufanya mikusanyiko isiyokuwa halali, hawapo mahakamani hapa na upande wa mashtaka hatuna taarifa zao hivyo, tunaomba hati ya kuwakamata washtakiwa hawa”alidai wakili Ester

Muda mfupi, baada ya Martin kuiomba mahakama hati ya kuwakamata washtakiwa hao, Wakili anayewatetea washtakiwa wote, Alex Massaba alidai kuwa huenda wateja wake wapo nje wanasubiri kuitwa kwa sababu hawajui kama kesi yao imehamishiwa kwa hakimu mwingine.

 “Mheshimwa hakimu, naiomba mahakama yako isitoe hati ya kuwakamata wateja wangu kwa sababu, huenda wateja wangu wanasubiri kuitwa kwa hakimu Godfrey Mwambapa ambaye ndio alikuwa anaiendesha kesi hii na hawana taarifa kama kesi hii imehamishiwa kwako,” amedai wakili wa utetezi, Massaba

 Pia wakili huyo aliomba upande wa mashtaka kuieleza mahakama ni lini itakamilisha upelelezi wa shauri hilo , ili kesi hiyo iweze kuendelea badala ya kutajwa kila siku.

 Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mushi alisema kwa kuzingatia maombi ya wakili wa utetezi, mahakama hiyo haitatoa hati ya kuwakamata washtakiwa hao, ila kama hawatafika mahakamani tarehe itakayopangwa, bila taarifa, mahakama hiyo itawakamata na kuwafutia dhamana.

 

 

 

Kwa pamoja wanadaiwa kuwa  Februari 16, mwaka 2018 huko Kinondoni katika eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni walifanya mkusanyiko usio wa halali na kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kuwa mkusanyiko huo ulikuwa na nia ya kufanya uvunjifu wa amani na kusababisha taharuki kwa wananchi.

 Kesi hiyo itatajwa tena Julai 12 mwaka huu.

Chanzo: mwananchi.co.tz